30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE KUFIKISHA KWA MAJALIWA SAKATA LA JKT WANAODAIWA KUUA

Na JANETH MUSHI,-ARUSHA

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Gipson ole Meseiyeki, amesema tukio la kuuawa kwa wakulima na wafugaji wanne linalodaiwa kufanywa na askari wa Suma JKT, atalifikisha kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ole Meseiyeki aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Kandaskirieti, Kata ya Olkokola, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wakati wa maziko ya wafugaji watatu wanaodaiwa kuuawa na askari hao, Januari 24 mwaka huu.

Alisema akirudi Dodoma atahakikisha anakutana na Waziri Mkuu, kuzungumza naye juu ya uonevu uliofanywa dhidi ya wananchi hao, lakini pia kuishauri Serikali kutenga maeneo ya malisho kwa mifugo.

“Nitakwenda kueleza kuhusu suala hili na tozo kubwa kati ya Sh 200,000 hadi 250,000 wanazotozwa wafugaji pale wanapokamatwa na mifugo katika misitu, achilia mbali ng’ombe waliokonda… nitaishauri Serikali juu ya mipango ya matumizi bora ya ardhi,” alisema.

Pamoja na hayo, mbunge huyo alisema wao hawajali waliotekeleza tukio hilo kwani hata wakifungwa au kunyongwa, mapengo waliyoyaacha marehemu hao ni makubwa na hivyo kuitaka Serikali kusaidia familia zilizoachwa, ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto.

Licha ya marehemu hao kutokuwa na dini, walizikwa kwa kufanyiwa ibada za mila.

Awali kabla ya mazishi, Mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Olkokola, Philemon Ndaskoi, aliwatia moyo wananchi hao na kuwataka wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Jitieni moyo, ila msisahau mwanadamu anaweza kufa kifo cha aina yoyote na hakuna anayejua atakufaje, kila mtu anatakiwa kujiandaa, yamkini hata vijana wetu hawakuweza kujua siku ya kuitwa, kifo hakichagui wewe ni mtu mashuhuri, masikini au tajiri, heri wafao katika Bwana,” alisema.

Awali familia za marehemu hao ziliiomba Serikali kuzitunza kwa madai kuwa kushitakiwa au kufungwa kwa waliohusika na mauaji hayo pekee hakuwasaidii.

Familia hizo pia ziliilalamikia Serikali kwa kupeleka msaada mdogo wa kilo 50 za mchele na nyama kilo 10 licha ya kusema kuwa inagharamia maziko.

Miili iliyochukuliwa jana kwa maziko ni pamoja na ya ndugu wawili; Mbayani Melau (27) na Lalashe Meibuko (25) pamoja na Seuri Melita (32) ambao wote walizikwa kijijini kwao Kandaskiriet, Kata ya Olkokola.

Mazishi hayo yalitanguliwa na yale yaliyofanyika juzi ya Julius Kilusu (49), aliyeacha wake watatu na watoto 12.

 Kaka wa marehemu Melau na Meibuko, Leowo Tengesi, alisema wamesikitishwa na kitendo cha askari kuamua kuwaua ndugu zao bila sababu ya msingi.

“Kama msitu ni mali ya Watanzania, basi inapotokea ukame kama huu wananchi waruhusiwe kukata majani kwa ajili ya mifugo na inapotokea wanawakuta watu huko wawachukulie hatua za kisheria na si kuwaua.

Kaka wa marehemu Amelita, Saning'o Lasubare, alisema mdogo wake ameacha mke na mtoto wa miezi tisa ambao alidai kuwa ni vema Serikali ikaangalia namna ya kuwasaidia.

Alisema mwili wa marehemu umekutwa una tundu la risasi kifuani upande wa kulia na ilibidi afanyiwe upasuaji iweze kutolewa.

Diwani wa Olkokola, Kalanga Laizer, alidai kuwa ukame ndio uliosababisha wananchi wake kuingiza mifugo katika shamba hilo la miti la Serikali.

Laizer alikanusha taarifa zilizodai kuwa wananchi walikuwa na silaha za jadi na walitaka kuwashambulia askari wa Suma JKT kwa kile alichoeleza kuwa lilikuwa ni kundi dogo la wananchi 14.

 “Huo msitu hakuna mpaka unaoonekana wa kutenganisha kijiji na msitu, hivyo wananchi wanaingiza mifugo huko wakati mwingine bila kujua kwani wanaochunga ni watoto,” alisema Laizer.

Alisema baada ya watoto kuona mifugo imechukuliwa, walitoa taarifa kijijini ambako walipiga kelele na kwamba kwa kawaida kelele hizo zinapopigwa, wanaume wote hutoka wakiwamo wazee ambao huwa ni uamuzi kwa majadiliano.

Laizer alisema wananchi walikuwa wanawafuata askari hao kwa lengo la kuomba walipishwe faini waweze kurejeshewa mifugo yao na si vinginevyo.

Alidai askari hao waliwagomea huku wakitaka walipwe faini ya sh 250,000 kwa ng'ombe kiasi alichodai ni kikubwa kuliko bei ya kununua ng'ombe mnadani ambayo ni sh 80,000.

Katikati ya wiki, askari wa Suma JKT wanadaiwa kuwapiga risasi na kuwaua watu wanne na kujeruhi wengine kadhaa katika  Kijiji cha Kandaskiriet, Kata ya Oldonyosambu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, kwa madai wananachi hao  walikuwa wanajaribu kuwanyang'anya  mifugo yao waliyoikamata katika operesheni maalumu ya kuiondoa ndani ya shamba la miti la Serikali la Meru Usa Plant.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles