Mbunge Kenya atolewa nje kwa kuingia na mtoto bungeni

0
591

NAIROBI, KENYA

MBUNGE mwanamke wa Kenya ametolewa nje ya Bunge jijini Nairobi, kwa kuingia na mtoto ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Mbunge huyo, Zulekha Hassan alisema  alipata dharura hivyo aliamua kwenda na mtoto wake katika kazi yake hiyo.

Zulekha aliingia akiwa amembeba mtoto wake wakati Bunge hilo likirushwa mubashara na Televisheni ya Taifa ya Kenya, KBC, na hivyo jambo hilo kuleta usumbufu.

Naibu Spika wa Bunge alijikuta katika wakati mgumu kuwadhibiti wabunge ambao baadhi walianza kupaza sauti huku wengine wakionekana wakizomeana.

Hata hivyo Naibu Spika alimtaka mwakilishi huyo wa wanawake katika Kaunti ya Kwale  kutoka nje  kwa kuwa kitendo hicho hakikubaliki.

Zulekha  baadae akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa alilazimika kuingia na mtoto wake bungeni kwa kuwa Bunge halijaandaa vyumba kwa ajili hiyo licha ya jambo hilo kukubaliwa tangu mwaka 2013.

Mbunge Zulekha Hassan

“Kiukweli nimejitahidi mno kutokuja na mtoto, lakini leo nilikuwa na dharura; ningefanya nini? Kama Bunge lingekuwa na sehemu ya kutunzia watoto au ya kuchezea watoto  ningeweza kumpelekea mtoto wangu huko,”.

“Sasa unapotaka wanawake wengi waje bungeni, unahitaji kutoa mazingira rafiki kwa ajili ya familia.” Alisema  Zulekha Hassan

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge la Kenya ” wageni” hawaruhusiwi ndani ya Bunge, wakiwamo watoto.

Kitendo hicho za Zulekha kuingia na mtoto Bungeni kimezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi wamempongeza mbunge huyo, wakizitaja na nchi nyingine kuruhusu watoto bungeni.

Lakini wengine waliandika kwenye Tweeter wakimshutumu Zulekha kutafuta ‘kiki’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here