28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Chadema amwaga machozi bungeni, aomba nafasi kujiunga CCM

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MBUNGE wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema), jana ameangua kilio bungeni akidai kwamba kumekuwa na uonevu mkubwa ndani ya chama chake na ameomba nafasi ya kujiunga na CCM mara baada ya Bunge kuvunjwa Juni 19.

Pia mbunge huyo amedai kwamba wabunge wa Chadema wamechangishwa zaidi ya Sh bilioni nane kugharamia Mfuko wa Uchaguzi na walipohoji waliambiwa kwamba fedha hizo zimetumika kujenga chama.

Akizungumza jana kabla ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, Lijualikali alisema Chadema mambo mengi hayaendi vizuri na mwenyekiti wa chama hicho amekuwa akikiendesha kidikteta.

“Watu wanaambiwa tumeingia kufuata posho, nimetukanwa sana, kama kuna watu wanawaza kuja hapa kwa ajili ya posho, mimi nimekuja hapa kwa ajili ya watu wa Kilombero. Nataka watu wajue hapakuwa na makubaliano na kulikuwa na amri na tulipohoji hakukuwa na majibu, hili ni agizo.

“Mheshimiwa Spika, tulihoji tunaenda karantini siku 14 na baada ya siku 14 tunarejea wapi. Unapotuambia turudi kwa hoja gani. 

“Mheshimiwa Spika, mimi nimeingia bungeni sijalala siku mbili maumivu, mimi nimekaa jela miezi sita, nimefungwa kwa sababu ya Chadema, leo nakuja kutimiza wajibu wangu naambiwa… (anaanza kulia).

“Mheshimiwa Spika, nimeumia ninapewa mashtaka kwenye redio, kwenye you-tube, hakuna barua ya kunishtaki, tunalilia katiba mpya, lakini katiba yetu tunaikanyaga.

“Tunalilia katiba ya nchi wakati ya kwetu tunaivunja, leo naonekana mtu wa ovyo kwa sababu nimekataa kitu ambacho naamini ni cha uongo,” alisema Lijualikali.

Alitolea mfano jinsi ambavyo mbunge wa CCM, Hussein Bashe alikuwa akiikosoa Serikali, lakini leo amekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, wakati hali ni tofauti kwa Chadema.

“Mungu ni mwema, hatuwezi kuwa chama cha demokrasia kama tunashindwa kufanya mambo madogo katika demokrasia, leo nakaa hapa nilikuwa namwangalia Bashe  anavyoikosoa Serikali, lakini leo Bashe ni Naibu Waziri.

“Tukipima demokrasia ndogo tu, hivi kesho tukifanya demokrasia katika nchi yetu tutafanya mangapi, wabunge wanakuja inbox mtutetee, wanashindwa kumwambia mtu ambaye hana dola kwamba unakosea mzee, hana jeshi hana polisi hana nguvu yoyote, akipewa dola itakuwaje?” alisema Lijualikali.

Alihoji zilipo zaidi ya Sh bilioni nane ambazo wabunge walikuwa wakikatwa posho kuchangia Mfuko wa Uchaguzi Mkuu wa chama.

“Mheshimiwa Spika, wakati naingia bungeni wabunge wote walilkuwa wanakatwa laki tano kila mwezi kwamba kutakuwa na Mfuko wa Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kampeni na sisi ni vijana tumejitoa kutumikia chama chetu.

“Mimi nilifanya ubunge nikiwa na milioni sita peke yake ili tuweze kuchangiana, tunakuja kuuliza tunaambiwa hela hakuna zaidi ya bilioni nane. 

“Unauliza mlisema tuweke hela kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, unajibiwa uchaguzi ni mchakato na tulinunua magari unauliza ruzuku imefanya kazi gani unaambiwa hii ni amri ya chama,” alisema Lijualikali.

Alisema katu hawezi kuendelea kuwepo katika chama hicho na atarudi Ifakara kufanya biashara.

“Mimi nipo tayari, nitarudi Ifakara nitalima mpunga nitafuga mbuzi, ng’ombe. Nitakuwa bodaboda, nitalima mchicha, mimi bado kijana, lakini siwezi kuendelea kutumika vibaya,” alisema Lijualikali.

Hata hivyo alisema kwamba kama CCM wapo tayari kumpokea yupo tayari kujiunga na chama hicho.

“Na Mheshimiwa Spika, niombe kama mtakuwa radhi kwa chama chako cha Mapinduzi (CCM), hata kazi yoyote nitafanya tu (wabunge wanashangilia). Nitaomba baada ya Bunge kuisha niwashukuru watu wa Kilombero,” alisema huku akianza kulia tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles