26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mbunge Chadema akalia kuti kavu  

james-oleNa Khamis Mkotya, Dodoma

SIKU mbili baada ya wabunge saba wa upinzani kufukuzwa bungeni kutokana na utovu wa nidhamu, mbunge mwingine wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amekalia kuti kavu.

Mbunge huyo, James Ole Millya yupo hatarini kusimamishwa vikao vya Bunge, iwapo kiti cha Spika hakitaridhika na ushahidi wake kuhusu ‘ushemeji wa Mhagama’.

Millya alipewa siku nne na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kuthibitisha madai yake kwamba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Jenista Mhagama ana undugu na mmoja wa wabia wa Kampuni ya Sky Associates inayomiliki mgodi wa Tanzanite One.

“Na sheria za kazi zinajulikana ni bahati mbaya kwamba mama yetu Mhagama naye anatajwa kwamba ni shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo. Dada anaitwa Asia Gonga ameolewa na Martin Mhagama au Yusufu Mhagama,” alisema Millya.

Baada ya Millya kutoa tuhuma hizo, Mhagama alisimama na kuomba mwongozo wa Spika, huku akimtaka mbunge huyo wa Simanjiro athibitishe maneno anayoyasema au afute kauli yake.

Kutokana na mbunge huyo kushindwa kufuta kauli, Dk. Tulia alimpa siku nne kuanzia Jumanne ya wiki iliyopita kuthibitisha ushemeji wa Waziri Mhagama na mtu ambaye alimtaja kwenye mawasilisho yake.

Akizungumza na MTANZANIA jana nje ya ukumbi wa Bunge, Millya alisema tayari amewasilisha ushahidi wake ofisini kwa Spika na kwamba iwapo hataridhika nao yupo tayari kwa jambo lolote litakaloamuliwa.

Kwa mujibu kanuni ya 63 ibara ndogo ya 8, Millya anaweza kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano, iwapo atashindwa kuthibitisha kauli yake baada ya muda aliopewa kupita.

Juzi Bunge liliwasimamisha kuhudhuria vikao vyake wabunge sita wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), baada ya kukutwa na makosa ya kudharau kiti na kufanya fujo bungeni.

Uamuzi huo ulikuja baada ya kuridhia mapendekezo ya adhabu yaliyotolewa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyowahoji wabunge hao kutokana na kufanya vurugu katika mkutano wa pili wa Bunge wa Januari 27, 2016 kuhusu matangazo ya Bunge ‘Live’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles