26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Chadema aja na hoja tano kumng’oa Mbowe

ASHA BANI Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema), ametangaza nia ya kumng’oa Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Freeman Mbowe katika nafasi hiyo endapo atapewa ridhaa na chama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam wakati akitangaza nia ya kuwania nafasi ya mwenyekiti, Mwambe alisema atahakikisha anamn’goa Mbowe na hoja yake kuu ni kuleta mabadiliko ndani ya Chadema.

Mwambe ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini, alisema nia ya kugombea ndani ya chama hicho si kuleta mgawanyiko kama ambavyo wamekuwa wakinukuliwa baadhi ya wana-Chadema katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine mbalimbali vya habari, bali ni kutaka kukitumikia chama na wanachama wake kwa uadilifu.

“Yamesemwa mengi juu ya nia yangu hii na watu wasio na nia njema na chama chetu, mimi binafsi na labda wengine kwa upeo wao mdogo wamesema mabaya wakiamini wako sahihi.

“Ndugu wanahabari, naomba muwafikishie ujumbe huu kuwa sina kinyongo nao hata kidogo, nawasamehe bila masharti yoyote, naona ni wajibu wangu kuendelea kutoa elimu juu ya hatua yangu hii,” alisema Mwambe.

Akitaja hoja ya pili, Mwambe alisema ameamua kugombea ili kuenzi na kuishi dhana ya demokrasia ambayo inabebwa na jina la chama hicho.

“Nchi yetu inazo sheria zinazompa kila mwananchi mwenye akili timamu fursa ya kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi, nimeamua nitekeleze haki hiyo bila kusukumwa na yeyote, aidha ninaamini katika ushindani,” alisema Mwambe.

Hoja ya tatu alisema ni wagombea wanatakiwa kuweka ahadi ambazo mwisho wa siku hutumika kuwapima na kwamba uchaguzi usio wa ushindani hutoa viongozi ambao mwisho wa siku hudai kuwa hakutaka ila alishurutishwa.

Mwambe alisema katika uchaguzi wowote ushindani hukuza ubunifu, umakini na kuongeza kuwa aliamua kuingia katika ushindani huo baada ya kuona mara kadhaa Mbowe akitangaza kutogombea tena nafasi hiyo, hivyo kuwa hoja yake ya tatu iliyomsukuma kuwania nafasi hiyo.

“Binafsi niliamua kuingia katika kinyang’anyiro hiki baada ya kuona kwamba Mbowe ametangaza mara tatu mfululizo na kutishia kuachia nafasi hiyo zaidi ya mara tatu, hivyo nikaona ipo haja ya kumpokea kijiti, hasa baada ya kueleza kwa kina madhila ambayo amepitia kwa vipindi vilivyotangulia,” alisema Mwambe.

Alisema baada ya kumsikia Mbowe akielezea madhila aliyopitia wakati wa uongozi wake, akaingiwa na huruma na kuamua kujigeuza kuwa ‘Simon wa Kirene aliyemsaidia Bwana Yesu Msalaba’.

 “Ninajua fika Mbowe amefanya mengi mazuri kwa chama chetu, ila kama binadamu huchoka na kuhitaji usaidizi, nimeamua kumsaidia na niwashukuru sana wale wote walioniunga mkono licha ya masimango na matusi yaliyoelekezewa kwangu,” alisema Mwambe huku akitumia maneno yaliyomo katika Biblia.

Alisema hoja yake ya nne ni kutaka viongozi waelewe uongozi ni dhamana na ukiomba hiyo dhamana na ukapewa ni vyema ukaithamini na ndiyo maana ameamua kugombea na kwamba isije tokea tena visingizio kwamba amelazimishwa.

Katika mkutano wake, Mwambe alisema hoja ya tano ni nia yake ya kuimarisha zaidi ngazi za chini za chama na huo ndio mtazamo wake aliouona.

Alisema uzito unaotolewa kwa sasa kwa ngazi za mikoa, wilaya na majimbo ni mdogo kulingana na umuhimu wa ngazi hizo katika ujenzi wa chama chenyewe na nafasi ya ngazi hizo katika mambo ya uchaguzi na kisiasa.

“Ninaamini nikipata fursa ya kuwa mwenyekiti wa chama changu nitajikita katika hili la kubuni na kupata njia mbalimbali za kuimarisha zaidi mikoa, wilaya na majimbo yetu kichama,” alieleza Mwambe.

Pia alizungumzia suala la ni kwanini hakutaka kutoa michango katika chama hicho kama ambavyo wenzake wamekuwa wakifanya.

Kwanza alisikitika kutokana na baadhi ya wana-Chadema kuvujisha nyaraka hizo za michango ambazo alisema hata yeye mwenyewe zilikuwa hazijawahi kumfikia kutoka makao makuu ya chama.

“Kuhusu nyaraka ambazo waandishi mnaniuliza za kutochangia chama, sikutaka kufanya hivyo kwa sababu chama kilikuwa na figisu za hapa na pale na waliosambaza nyaraka hizo walivujisha makusudi ili nisigombee uchaguzi,” alisema Mwambe.

Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kufahamu endapo akishindwa uchaguzi huo kama atarudi CCM alikokuwa awali, alisema hawezi kurudi na wala hajafikiria kufanya hivyo.

Mwambe alifika mbali baada ya mwandishi (si wa MTANZANIA) kumuuliza kwamba aliambiwa juzi alikutana na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kumpanga ili achukue fomu ya kumwondoa Mbowe, alisema yeye hapangiwi kuwa na rafiki yeyote.

Alisema ikumbukwe kwamba Sumaye ni rafiki na mtu ambaye anafanya naye kazi na kumuheshimu, hivyo suala la kukutana naye ni la kawaida na kwamba huwa anakutana naye kuomba ushauri mbalimbali.

“Lakini mkumbuke kwamba mimi sipangiwi na mtu rafiki yeyote wa kuzungumza naye au kukaa naye, hivyo kukaa na Sumaye sio kwa ajili ya kumuomba kugombea, hapana, ni kubadilishana mawazo kama ambavyo wao pia wanakaa.

“Najua nafuatiliwa sana kila hatua yangu, lakini namuachia Mungu ndiye ambaye atanilinda, wala siogopi na kwamba kuna sheria ambazo zipo tunalindwa, na kila mtu ana haki ya kuishi, hivyo sifikirii kwamba naweza kufanyiwa ubaya wa aina yoyote,” alisema Mwambe.

Hata hivyo alisema yeye ni mgombea kama ambavyo wanafanya wengine na anaamini atakuwa mwenyekiti kwa kuwa pia ameshapata baraka za wazee.

Chadema kwa sasa iko katika hatua ya kufanya uchaguzi ndani ya chama hicho  kwa nafasi ya Mwenyekiti na uchaguzi wa kanda ambapo tayari mpambano huo umeanza kuibua sura mpya baada ya baadhi ya wagombea kuanza kurushiana maneno.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles