GUSTAPHU HAULE – PWANI
MBUNGE wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa (CCM), amewataka wenyeviti wa Serikali ya Vijiji na Vitongoji waliochaguliwa hivi karibuni jimboni humo kuhakikisha wanakwenda kutekeleza majukumu yao kuendana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli.
Kauli hiyo alitoa kauli hiyo juzi katika hafla ya kuapishwa kwa wenyeviti hao iliyofanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi, chini ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Namwike Mbaba.
Aliwataka wenyeviti hao kuwa kiapo walichokiampa kitadumu ndani ya miaka mitano kwahiyo lazima waende kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
Alisema ili waweze kupata maendeleo ni lazima wafanyekazi kulingana na kasi ya Rais Dk.Magufuli na kwamba wakiweza kwenda na kasi hiyo upo uhakika wa halmashauri yao kukua kiuchumi.
“Serikali hii inataka kasi na mmeona kasi ya Rais Magufuli na kazi anazofanya, kwa hiyo kama spidi itakuwa kubwa na kazi itakuwa kubwa tena yenye mafanikio,” alisema Jumaa
Mbunge huyo alisema kuwa Rais Magufuli hawezi kupita kila kijiji na vitongoji kwa ajili ya kutatua changamoto na kero za wananchi na badala yake wao ndio waliopewa dhamana katika maeneo yao kwahiyo ni lazima wamsaidie Rais katika kutekeleza mipango yake.
“Rais Magufuli anatekeleza miradi mikubwa yenye faida kwa Watanzania wote lakini sisi tuliochini hasa ninyi wenyeviti wa vijiji lazima tumuonee huruma kwa kuhakikisha tunamsaidia kutatua kero ndogondogo zilizopo katika maeneo yenu,” alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mansour Kisebengo, alisema wenyeviti hao wanapaswa kuitunza heshima waliyopewa kwakuwa tegemeo la Wananchi lipo mikononi mwao.