23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge CCM akosoa elimu bure

HusseinBasheGrace Shitundu na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), amesema sera ya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari inayotekelezwa na Serikali haikuwa na maandalizi ya kutosha.

Bashe ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, aliyasema hayo wakati akichangia ripoti ya utafiti wa utekelezaji wa sera mpya ya elimu bure ambayo ilizinduliwa na Taasisi ya Twaweza Dar es Salaam jana.

Alisema kutokana na kukosa maandalizi, ni vyema kurudi mezani na kuangalia upya namna ya kuiweka sera hiyo kwa kuhakikisha inapatikana elimu bure iliyo bora.

Kutokana na changamoto hizo, Bashe alisema kuwa ndoto ya kuwa na Tanzania yenye viwanda haitaweza kutimia endapo tatizo la elimu halijatatuliwa.

“Kama Taifa tupo katika tatizo, ni vizuri kukiri kuwa tumefanya makosa kuingia kwenye sera ya elimu bure bila maandalizi, kwani Serikali kupeleka mabilioni si kutatua tatizo.

“Ni vyema kuangalia tunataka kutengeneza taifa la aina gani, hapo ndiyo tutaweza kujua tunaweka sera ya elimu ya aina gani na hilo limefanywa na nchi nyingi ambazo zimeendelea katika sekta hiyo ikiwamo Cuba,” alisema.

Bashe alisema kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikiangalia ukuaji wa elimu kwa mlengo wa wingi wa wanafunzi kuanza darasa la kwanza na kusahau ubora wa elimu wanayopata.

Alisema mawaziri wote waliowahi kuwa katika Wizara ya Elimu kuanzia mwaka 2006 akiwamo Magreth Sitta, Jumanne Maghembe na Shukuru Kawamba katika hotuba zao walikuwa wakizungumzia kukua kwa elimu kwa misingi ya wingi wa wanafunzi.

“Na wanapokuwa wanazidi, mtindo wa kuwapunguza unaotumika ni mitihani ambayo ndiyo inakuwa kipimo cha nani andelee na shule na nani abaki,” alisema Bashe.

Pia alisema jamii isitegemee kupata matokeo mazuri endapo sekta ya elimu itaendelea kugeuzwa dampo la kuwatumia waliofeli kwa kuwafanya walimu.

“Imekuwa ni kawaida kwa wanafunzi waliofeli kidato cha nne na sita kukimbilia katika ualimu. Je, tunategemea watoto wanaofundishwa na hao waliofeli nao watafaulu?

“Jamii imejijengea mawazo kuwa umasikini unaondoka kwa kuwa na miundombinu mizuri, umeme wa uhakika na simu za mkononi jambo ambalo si kweli bali ni kuwa na elimu bora,” alisema Bashe.

Naye Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Joviter Katabaro, alisema Rais Dk. John Magufuli alikuwa na nia nzuri na sera hiyo ya elimu bure, lakini inaonyesha washauri wa mambo ya elimu hawakufanya kazi yao ipasavyo.

Alisema michango iliyokuwa ikichangwa na wazazi ilikuwa ikisaidia katika mambo mbalimbali ambayo kwa sasa fedha ya ruzuku haikidhi kwani kuna shule zilizokuwa zikiweka uji kwa ajili ya kuwashibisha watoto.

“Elimu haiwezi kuwa bora kwenye tumbo ambalo halina kitu, hivyo mwanafunzi mwenye njaa hawezi kufanya vizuri kulinganisha na yule ambaye amekula,” alisema.

Alisema ingekuwa ni afadhali wangeendelea kulipia hizo Sh. 20,000 za ada na Serikali ingekuwa na kazi ya kuwalisha wanafunzi.

Pia Dk. Katabaro aliishauri Serikali kuangalia upya suala la shule binafsi kwani imekuwa ni chanzo kikubwa kwa kutengeneza tabaka katika jamii.

“Watoto wanaosoma shule za binafsi wanaishi maisha tofauti kabisa na wale wa shule za umma, huwezi kumfananisha mtoto anayenyeshewa na mvua au kugombea daladala wakati wa kwenda shule na yule anayefuatwa na basi la shule nyumbani,” alisema.

Awali akizindua ripoti hiyo, Profesa Kitila Mkumbo alisema inaonyesha zaidi ya asilimia 90 wanafahamu juu ya elimu bure na asilimia 88 wanaamini kuwa inaweza kutekelezeka.

Alisema pamoja na Serikali kupeleka ruzuku shuleni, bado michango ya wazazi ilikuwa inasaidia zaidi kwa kuwa ilikuwa ni mikubwa kulinganisha na fedha zinazopelekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles