29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mbunge CCM aigeuka Serikali

Peter SerukambaNa Khamis Mkotya, Dodoma

BAADHI ya wabunge wamekosoa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango.

Wakichangia bungeni jana, wabunge hao walisema mpango huo hauwezi kufanikiwa pasikuwapo na juhudi za ziada na wengine wakisema una nia ya kuua mashirika ya umma na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, Serikali kupitia mpango huo imepiga marufuku utaratibu wa kutumia sehemu ya maduhuli (retention), hivyo mapato yote yatakayokusanywa na halmashauri na mashirika ya umma  yatawasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali (Hazina).

Akichangia mjadala wa mpango huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM), aliwataka wabunge wenzake kuungana   kupinga uamuzi huo wa Serikali, akisema unalenga kuua halmashauri  na mashirika ya umma.

“Utaratibu wa kufuta retention scheme sikubaliani nao, mambo haya ndiyo yaliua viwanda vyetu miaka iliyopita kwa sababu walikuwa wakitaka kufanya hata matengenezo ya mashine wanashindwa hawana fedha, fedha zote zimehifadhiwa Hazina.

“Leo mnataka kuua halmashauri jambo hili haliwezekani, wabunge tupinge ‘retention scheme’ Serikali mnataka kuyapeleka wapi mashirika ya umma?

“Yaani leo Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa) likikusanya fedha zote ziende Central Government (Serikali Kuu), mtaua mbuga zetu kwa utaratibu huu. Kama ni fedha za Serikali sawa wekeni Hazina, lakini fedha zinazozalishwa sehemu nyingine ziacheni zibaki huko,” alisema.

Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii, alisema uamuzi huo unakinzana na dhana ya ugatuaji wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa (Decentralization).

Mbunge huyo pia alizungumzia suala la ujenzi wa reli mpya na kuitaka Serikali kuainisha katika bajeti ya mwaka huu ujenzi wa reli mpya katika kiwango cha Standard Gauge  kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma itajengwa lini.

“Katika mpango huu naona suala la ujenzi wa reli limewekwa kijumla jumla tu, nataka mtuambie ujenzi huu wa reli mpya kwa kiwango cha ‘Standard Gauge’ kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma, Kaliua hadi Mpanda au ni kutoka wapi kwenda wapi?” alihoji.

 

Bashe

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), akizungumza nje ya viwanja vya Bunge, alisema msimamo wa wabunge kanda ya magharibi mwaka huu ni kupigania reli.

“Hilo tumelisema wazi,   tutakwamisha bajeti ya mwaka huu kama Serikali itashindwa kukamilisha ahadi yake ya kujenga reli mpya kwa kiwango cha Standard Gouge. Tumesema bila reli no bajeti.

“Hili limekuwa likisemwa kwa muda mrefu lakini utekelezaji wake hakuna, reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, Tabora hadi Mwanza, Kaliua hadi Mpanda na Uvinza hadi Msingati,” alisema.

 

Gekul

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), alisema uamuzi wa Serikali wa ‘retention’ hauna tija na ni uamuzi wa kutaka kuua halmashauri   nchini.

Gekul alisema  uamuzi huo unairudisha nchi katika historia ambako mwaka 1982 Serikali iliamua kugatua madaraka na kuyashusha chini, kwa vile mpango  wa zamani wa kila kitu kuwa Serikali Kuu ulikuwa na madhara.

“Utaratibu huu utaua halmashauri zetu, lazima tujue Serikali za Mitaa zina mamlaka yake, huko wanaajiri wenyewe na wanakusanya wenyewe leo kusema makusanyo yote lazima yaende Hazina ndiyo waanze kuwapimia wakati wamekusanya wenyewe, hii si sawa.

“Inakuwaje wakusanye wengine halafu wapange wengine? Kwa mtindo huu maendeleo yatakuwa hayapo huko chini, hili jambo litapunguza hata morali kwa wanaokusanya huko chini.

“Mwalimu Nyerere aliliona hili tangu mwanzo ndiyo maana mwaka 1982 aligatua madaraka ya Serikali Kuu yakaenda Serikali za Mitaa  kwa sababu alijua Serikali haiwezi kufanya kila kitu,” alisema.

 

Sakaya

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF)  alisema licha ya Rais Magufuli kuahidi kuwa anataka Tanzania iwe nchi ya viwanda, lakini haoni dalili za kufikia huko.

Alisema ni aibu kwa Tanzania kugeuzwa soko la bidhaa za nchi nyingine  na akaeleza kukerwa na kukosekana kwa juhudi za kudhibiti matumizi ya dola.

“Tunasema tunaka Tanzania ya viwanda, itawezekanaje wakati tumeshindwa kudhibiti matumizi ya dola, hakuna nchi ambayo wananchi wanapata huduma kwa dola.

“Ni Tanzania tu watu wanapata huduma madukani kwa dola, kuna utitiri wa maduka ya chenji, ukienda Kariakoo watu wana dola mikononi, machinga tu wanatembea na dola mikononi hii ni nchi gani?,” alihoji.

Kuhusu viwanda alisema: “Mnasema nchi ya viwanda, viwanda vyenywe vipi?  Tulikuwa na viwanda vingi tu vyote vimekufa, hatuwezi kufika huko ikiwa hata tooth pick (vijiti vya kuchokonolea meno) tunaagiza nje, this is a shame (ni aibu).

“Hii mipango ni mizuri lakini tusipojitahidi kubadilisha mindset (mtazamo) za watendaji itakuwa kazi bure kwa sababu mipango hii haiendi kutekelezwa na robot   inakwenda kutekelezwa na watu,” alisema.

 

Hasunga

Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema mpango huo utafanikiwa iwapo watendaji wa Serikali watavaa uzalendo wakafanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.

Alisema  Tanzania ina fursa nzuri za maendeleo lakini maendeleo hayapo kutokana na kukosa viongozi wazalendo.

“Tanzania tunayo ardhi nzuri, misitu, madini, mbuga, mito, maziwa, bahari lakini pia watu ni wengi takriban milioni 50.

“Tuna faida za ziada, lakini hatuwezi kufikia nchi ya kipato cha kati kwa sababu tatizo ni viongozi. Nashukuru leo tumempata kiongozi mzuri, Rais Magufuli, naamini tutasogea,” alisema.

Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mwelekeo wa bajeti katika kipindi cha mwaka 2016/2017 uliwasilishwa bungeni juzi, huku ukiweka mkazo katika ukusanyaji wa mapato na kubana matumizi.

Mwelekeo huo unaonyesha kuwa  bajeti itaongezeka kutoka Sh trilioni 22.495 mwaka 2015/2016 hadi Sh trilioni 22.991 mwaka 2016/2017, ambalo ni   ongezeko la asilimia 2.2.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles