NA KULWA MZEE-DODOMA
MBUNGE wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM) amehoji kwa nini Serikali inatoza kodi kwenye shisha wakati imepiga marufuku kutumika.
Aeshi alisema hayo jana bungeni alipochangia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.
“Shisha ni haramu…. au ni dawa za kulevya?” alihoji Aeshi.
Alisema kama ni haramu inatumika vibaya hata sigara inatumika vibaya kwa sababu kuna watu wanaotumia kwa kuchanganya na bangi.
Alisema shisha imezuiwa Dar es Salaam peke yae lakini katika mikoa mingine kama Arusha na Dodoma biashara hiyo inaendelea.
“Kama shisha haramu iondolewe katika kutozwa kodi, polisi ndiyo wenye wajibu wa kudhibiti kama inatumika vibaya, mikoa yote inatumika kasoro Dar es Salaam tu ndiko imezuiliwa.
“Serikali iliangalie suala la shisha kwa sababu wafanyabiashara wanalipa kodi,”alisema.
Mwishoni mwaka jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipiga marufuku uvutaji wa shisha nchini na kulitaka Jeshi la Polisi kufuatilia na kutokomeza matumizi ya sigara hiyo kuokoa makundi ya vijana ambao wanajihusisha na ulevi huo.
Akizungumzia kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa bandarini, Aeshi alisema ianze kutozwa baada ya siku 30 kwa sababu siku saba zilizopendekezwa hazitoshi.
“Ukitaka kurekebisha kitu rekebisha moja kwa moja, siku saba ziongezwe ziwe 30, Bandari ya Dar es Salaam kila siku mtandao uko chini,”alisema.
Mbunge wa Micheweni, Rashid Ally Abdallah (CCM) alizungumzia nidhamu katika matumizi ya fedha zinazotengwa katika bajeti ya maendeleo.