32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge CCM afariki dunia ghafla

Na ANDREW MSECHU -DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Newala Vijijini, Rashid Akibar (CCM),  amefariki dunia ghafla mkoani Lindi.

 Taarifa za kifo cha mbunge huyo zilisambaa jana mchana, ikielezwa kuwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Mingoyo, Halmashauri ya Lindi Vijijini na mwili wake ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Sokoine mkoani Lindi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Predunciana Protas, alithibitisha kutokea kifo cha mbunge huyo katika nyumba ya kulala wageni Mingoyo anayoimiliki.

Hadi kufikia jana saa 12 jioni, Kamanda Protas alisema Jeshi la Polisi linasubiri taarifa za uchunguzi wa daktari kisha watatoa taarifa kamili.

“Nilikuwa nje ya mji na sasa ndiyo narudi mjini, ila ni kweli, hata mimi nimepata hizo taarifa ambazo nikifika ofisini ndiyo nitaweza kueleza kwa undani,” alisema Kamanda Protas.

BUNGE LAMLILIA

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, ilimnukuu Spika wa Bunge, Job Ndugai akieleza kuhusu kifo cha mbunge huyo na kutoa pole kwa wafiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya mbunge huyo.

“Natoa pole kwa wafiwa wote wakiwemo familia ya marehemu, wabunge, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema Ndugai kupitia taarifa hiyo.

CCM NA POLE

Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mtwara, kupitia kwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa mkoa, Selemani Sankwa, pia kimetoa taarifa kuhusu kifo cha mbunge Akbar.

Sankwa alisema CCM imepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha mbunge huyo.

Alisema kifo cha mbunge huyo kilitokea Mnazi Mmoja mkoani Lindi.

 “CCM inathamini na kutambua mchango mkubwa wa marehemu enzi ya uhai wake akiwa mbunge katika kuwatumikia wananchi wa Newala Vijijini na katika kukijenga Chama Cha Mapinduzi.

“Aidha taarifa za mazishi zitatolewa baada ya makubaliano ya familia na Ofisi ya Bunge.

“CCM inatoa pole sana kwa wafiwa na inawatakia subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina,” alisema Sankwa.

MCHANGO WAKE BUNGENI

Moja ya michango yake ya kukumbukwa aliyowahi kuitoa bungeni ni ule wa Mei 31, 2018 pale alipochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/19 jijini Dodoma. 

Akitoa mchango wake, Akbar aliwataka mawaziri wa madini kwenda Afrika Kusini kuwatafuta ‘masangoma’ (waganga wa kienyeji) wathibitishe kama kweli madini yanatokana na majini ili Watanzania waipate kwa wingi rasilimali hiyo.

Akbar alisema kuwa hadhani kama Rais Dk. John Magufuli, ameipenda wizara hiyo kwa kuipa mawaziri watatu bali anataka ilete matokeo mazuri.

“Nimewahi kusikia kuwa madini yanatokana na majini, kama ni kweli muende South Afrika (Afrika Kusini) mkatafute sangoma ili na sisi tupate madini,” alisema Akbar.

Alisema kutokana na utendaji mbovu wa Shirika la Madini nchini (Stamico), angekuwa yeye angelivunja kwa kushindwa kufanya kazi.

“Stamico itaendelea kuwa mzigo kwetu, tuivunje,” alisema Akbar.

Kauli ya kutaka Stamico ivunjwe iliungwa mkono na Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali (CCM), ambaye alisema kuwa waendelee kuipa fedha kwa majaribio.

Alisema badala ya shirika hilo kuleta faida, linaleta hasara huku kampuni binafsi za madini zikizalisha faida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles