Mbunge CCM achangiwa milioni 2/- fomu ya ubunge

0
298

Na Walter Mguluchuma-Katavi

WANANCHI wa Jimbo la Mpanda Vijijini wilayani Tanganyika mkoani Katavi, wamemchangia mbunge anayemaliza muda wake, Moshi Kakoso zaidi ya Sh milioni mbili kulipia fomu ya kugombea ubunge tena katika jimbo hilo.

Michango hiyo alikabidhiwa juzi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake wakati wa kukabidhi kiasi hicho cha fedha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila, Ally Mashaka alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo wameamua kumchangia kutokana na mambo makubwa ya maendeleo yaliyofanyika.

Alisema kuwa wananchi bado wana imani kubwa  na kazi zilizofanywa na mbunge huyo ambaye anamaliza muda wake.

Alifafanua kuwa vijiiji ambavyo vimemchangia fedha hizo vinatoka katika Tarafa za Kabungu, Karema na Mwese.

Mashaka alisema mafanikio yaliofanyika kwenye jimbo hilo kwenye uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ni mengi na wala si rahisi kuyaelezea yote. 

 Kwa upande wake, Kakoso alisema kuwa  kiasi hicho walichomchangia ni kikubwa kwani fedha zinazohitajika kuchukulia fomu za wagombea ubunge ndani ya CCM ni Sh 100, 000.

Aliwashukuru kwa upendo wao kwake kwani hatua hiyo imemtia moyo na kujiona ana deni zaidi la kuchochea maendeleo kwa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here