24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Bonnah awakosha wananchi Tabata

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wananchi wa Kata ya Tabata wanaotakiwa kuhama kupisha mradi wa mabasi yaendayo haraka ‘mwendokasi’ wametakiwa kuendelea kuishi na kuendeleza makazi yao mpaka awamu ya sita ya ujenzi huo itakapoanza kutekelezwa.

Nyumba za wananchi hao ziliwekwa alama ya X kwa muda mrefu hatua iliyosababisha kushindwa kuendeleza makazi yao wakisubiri kutekelezwa kwa mradi huo.

Ujenzi wa Soko la Tabata Muslim ukiendelea.

Akizungumza Julai 22,2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amesema awamu ya sita ya mradi huo imepangwa kutekelezwa katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo ikiwemo Kata ya Tabata lakini mipango ya utekelezaji bado haijaanza.

“Sasa hivi mradi wa mwendokasi uko awamu ya tatu mpaka waje wafike awamu ya sita siyo leo, kwahiyo endelezeni makazi yenu mpaka serikali itakapokuwa tayari kuanza mradi huo,” amesema Bonnah.

Diwani wa Kata ya Tabata, Omary Matulanga, amesema wananchi wengi walikuwa wanashindwa kuendeleza makazi yao kutokana na nyumba zao kuwekwa alama ya X kwa miaka sita hali iliyoibua malalamiko kila siku.

Katika mkutano huo pia baadhi ya wananchi wamelalamikia kukosekana kwa huduma ya maji ambapo Dawasa wameahidi kufuatilia maeneo yote yenye changamoto kuanzia leo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Msimbazi, Godfrey Kizigo, ameomba barabara ya kuanzia sokoni Muslim kuzunguka Comfort na kukutana na ile ya Tabata shule yenye urefu wa mita 450 ijengwe ili kuwaondolea kero wakazi na wafanyabiashara wa soko hilo.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya Kata ya Tabata. Kulia ni Diwani wa kata hiyo, Omary Matulanga.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Said Sidde, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amempongeza Bonnah kwa kupigania maendeleo ya Jimbo la Segerea.

“Mheshimiwa mbunge anatimiza matakwa ya katiba ya kuchaguliwa, anakwenda kwa wananchi kuwaeleza mipango inayofanyika ya kuwaletea maendeleo na kupokea changamoto zao. Tunapongeza viongozi wanakuja kuonana na wananchi ili tuhakikishe ahadi tulizoahidi kwa zinatekelezwa,” amesema Sidde.

Mbunge huyo tayari amefanya ziara na mikutano ya hadhara katika Kata za Liwiti, Kimanga, Kipawa na Tabata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles