23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Bonnah apiga kambi jimboni kusikiliza, kutatua kero za wananchi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli amefanya ziara kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mitaa na kata mbalimbali za jimbo hilo kwa lengo la kutatua kero walizonazo.

Bonnah yuko jimboni tangu Bunge la Bajeti (2024/2025) lilipohitimishwa ambapo amekuwa akitumia muda wa mapumziko kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukutana na wananchi na kusikiliza kero walizonazo kisha kuzitolea majibu.

Katika ziara zake amekuwa akiambatana na madiwani wa kata husika, wajumbe wa kamati za siasa wa kata, maafisa watendaji wa kata na wataalam mbalimbali wa serikali ili kutolea ufafanuzi wa kero zinazoibuliwa na wananchi.

Julai 18,2024 mbunge huyo amefanya ziara katika Kata ya Kipawa yenye mitaa sita yaani Uwanja wa Ndege, Mogo, Karataka, Mji mpya, Kipunguni na Sitakishari ambayo ilifuatiwa na mkutano wa hadhara uliofayika katika Mtaa wa Mogo.

Baadhi ya kero zilizowasilishwa na wananchi ni maji kujaa kwenye makazi yao kulikosababishwa na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kukosekana kwa vivuko vya waenda kwa miguu, vumbi, kukosekana kwa soko, ubovu wa miundombinu ya barabara, madaraja, mifereji, upatikanaji maji safi na salama pamoja na mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Mkazi wa Mtaa wa Mogo Cecilia Daniel, amesema usalama wa watoto wanaopita katika daraja la juu uko shakani na kuomba kiwekwe kivuko kitakachowawezesha kuvuka kirahisi.

“Tumeishi maeneo haya zaidi ya miaka 40 hakukuwa na maji yaliyokuwa yanaingia kwenye makazi yetu, lakini tangu walipojenga mradi wa reli ya kisasa maji yanaingia kwenye makazi yetu, tumekuwa ni wahanga badala ya kufaidika na mradi,” amesema mkazi wa Mogo, Absalum Msuya.

Wananchi hao pia wameiomba Serikali kurejesha mikopo ya kuunganisha maji ili waweze kupata huduma hiyo huku wakiendelea kulipa madeni taratibu.

Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, amesema katika Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kata hiyo imetengewa zaidi ya Sh bilioni sita ambazo zitasaidia kujenga madaraja, mifereji na barabara ikiwemo ya Simba Oil – Stakishari Polisi – Semirani.

“Soko ni mojawapo ya kipaumbele chetu, tumeanza mchakato wa kutafuta eneo katika Mtaa wa Karakata, wananchi wameshakubali kulipwa fidia na Sh milioni 200 zimetengwa,” amesema Kwezi.

Kuhusu kero ya mikopo Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amesema wametenga zaidi ya Sh bilioni 11 kukopesha wanawake, vijana na wenye ulemavu na kuwataka watakaonufaika kuwa waadilifu katika urejeshaji ili watu wengine waweze kukopa.

Kwa upande wake Bonnah amesema amedhamiria kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanaondokana na kero walizonazo ambapo amekuwa akiziwasilisha bungeni na kutengewa bajeti huku nyingine zikitatuliwa kupitia fedha za mfuko wa jimbo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amepongeza juhudi za mbunge huyo katika kuwaletea wananchi wake maendeleo na kusema viongozi kama hao ndio chama kinawahitaji.

“Chama Cha Mapinduzi aina ya viongozi kama hawa ndio tunawahitaji, wanaojua shida ndio wanaoweza kuzitatua hivyo, muendelee kukiamini chama chetu tupo kazini,” amesema Sidde.

Amesema mkataba baina ya chama hicho na wananchi ni wa miaka mitano na kwamba bado wanaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali kuhakikisha zinapungua au kumalizika kabisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles