27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Bonnah akomalia ujenzi Bonyokwa sekondari

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, ameiomba Serikali kumpelekea fedha mkandarasi ili aongeze kasi ya ujenzi katika Shule ya Sekondari Bonyokwa.

Bonnah ametoa kauli hiyo Januari 15,2024 wakati wa ziara yake katika Kata za Bonyokwa, Liwiti na Mnyamani kukagua miradi ya maendeleo.

Amesema katika jimbo hilo ujenzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari unaendelea lakini Bonyokwa umechukua muda mrefu.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli (katikati) akitoka kukagua ujenzi katika Shule ya Sekondari Bonyokwa.

“Shule itapendwa kutokana na ufaulu ambao unachangiwa na kuwepo kwa miundombinu mizuri, tutahakikisha tunafuatilia ili ujenzi huu ukamilike haraka shule iwe na miundombinu mizuri,” amesema Bonnah.

Mbunge huyo pia ameahidi kuipatia shule hiyo mashine ya kurudufu maandishi (photocopy) ili kurahisisha uandaaji wa mitihani kwa wanafunzi.

Amesema mwaka 2023 kupitia Mfuko wa Jimbo walinunua mashine hizo katika Shule ya Sekondari Kisungu na kwamba mwaka huu wanatarajia kununua katika Shule ya Sekondari Kimanga na nyingine.

Kuhusu Shule ya Sekondari ya Liwiti licha ya kuridhishwa na kasi ya ujenzi ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi huo lakini akashauri ujengwe uzio ili watoto waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli (Kushoto) akiwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Liwiti alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike, Malilo, amesema changamoto ya malipo kwa mkandarasi imechangia kusuasua kwa ujenzi lakini jitihada zinafanyika aweze kulipwa ili aendelee na kazi.

Amesema ujenzi huo ulianza Desemba 2022 na mkataba uliisha Desemba 2023 lakini mkandarasi ameomba kuongezewa muda hadi Machi 2024.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bonyokwa, Hidaya Makabu, amesema wamepangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza 495 na kati yao walioripoti ni 176.

Amesema idadi ndogo ya wanafunzi walioripoti imechangiwa na umbali wanakotoka wanafunzi hatua iliyosababisha baadhi ya wazazi kufanya jitihada za kuwahamisha shule za karibu.

“Wanafunzi wa Kifuru wanalazimika kupanda magari mawili na bajaji na wakati mwingine bodaboda, wazazi wanaona ni changamoto hivyo wanajaribu kutafuta shule za karibu kama Kisungu au Kinyerezi ambako mwanafunzi anaweza kupanda gari moja,” amesema Makabu.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Liwiti, Daudi Ng’wandu, amesema jengo la sakafu tano lililoanza kujengwa Juni 2022 liko kwenye hatua za mwisho kukamilika na tayari wamepokea wanafunzi 370 wa kidato cha kwanza.

Kwa mujibu wa mkuu huyo, ujenzi huo umegharimu Sh bilioni 1.8 ambazo ni mapato ya ndani ya halmashauri na zingine kutoka Tamisemi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles