22 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Mbunge ataka sheria kudhibiti deni la taifa

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda (Chadema) amesema kutokana na deni la taifa kuendelea kukua, ni vyema ikawekwa sheria itakayoibana Serikali kukopa hadi pale itakapopata idhini ya Bunge.

Mwakagenda alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akichangia mjadala wa mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21.

Mbunge huyo alisema deni la taifa kwa sasa limevuka Sh trilioni 50, hivyo akataka kuwe na sheria Serikali isikope hadi Bunge liridhie kwani deni hilo linazidi kuwa kubwa. 

“Deni la taifa tumevuka trilioni 50/-, tuweke sheria Serikali isikope hadi Bunge liridhie, deni limekuwa kubwa, mna lugha zenu za kisomi kwamba ni himilivu, wakati linazidi kuwa kubwa,” alisema Mwakagenda.

Aidha Mwakagenda alisema kuna haja ya Serikali kuwaangalia walimu kwani nyumba wanazoishi hazina ubora huku akisisitiza suala la ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule. 

“Nyumba za walimu hiki ni kilio kikubwa, walimu wengi wamepanga, hebu waziri tuwaangalie walimu, matundu ya vyoo kwa watoto wa kike nalo hili tunatakiwa kuliangalia,” alisema.

Mwakagenda alihoji ni kwanini Bunge linapitisha fedha, lakini wizara zimekuwa zikipata chache hali ambayo imekuwa ikisababisha mambo mengi kukwama.

“Tunapopitisha fedha wizara nyingi zinapata robo ya mapato, mtuambie kwamba Serikali haina hela, lakini Serikali ya awamu ya tano, inasema ina hela, kwanini Bunge linapitisha fedha, lakini sehemu husika zinafika kidogo? Waziri Mpango naomba usimamie hili,” alisema Mwakagenda. 

Pia mbunge huyo alisema kwamba hakuna maendeleo bila demokrasia, hivyo kuna haja ya Serikali kuliangalia jambo hilo kwa umakini.

“Hali ya demokrasia kwa sasa haipo vizuri, Mheshimiwa Mwenyekiti hakuna maendeleo bila demokrasia, leo tunapanga mipango tunaendeleaje, tukae chini kama taifa, tuache woga. Leo hii mnaumiza watu wengi na watu wanaona suala la kujiandikisha sio muhimu wala la msingi. 

“Mmepitisha watu ambao hatujawapenda, tunapataje maendeleo? Demokrasia ni muhimu sana,” alisema Mwakagenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles