23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Mbunge ataka mkoa mpya wa Tanesco Mbagala

Na Ramadhani Hassan, Dodoma

MBUNGE wa Mbagala, Issa Mangungu (CCM) amehoji ni lini Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litaanzisha Mkoa wa Tanesco Mbagala kutokana na kuzidiwa na wateja.

Akiuliza swali jana bungeni, Mangungu alidai jimbo hilo lina wakazi zaidi ya 800,000 na Tanesco Wilaya ya Mbagala ina wateja zaidi ya 400,000 mara nne zaidi ya baadhi ya mikoa ya ki-Tanesco.

Alihoji ni lini Serikali itaanzisha Mkoa wa Tanesco Mbagala ili kukabiliana na changamoto za umeme zilizopo na kuongeza ufanisi.

Pia alihoji ni lini usambazaji wa umeme utakamilika katika maeneo ya Kilimahewa, Changanyikeni na Vikunai Kata ya Toangoma; Mponda, Vigozi na Churuvi Kata ya Mianzini.

Ikijibu swali hilo, Wizara ya Nishati ilieleza kuwa ofisi ya Tanesco Wilaya ya Mbagala ipo katika Mkoa wa Tanesco Temeke.

Ilieleza kiutendaji, Tanesco Wilaya ya Mbagala inahudumia kata tisa zenye mitaa 56 maeneo ya Chamazi, Charambe, Kibondemaji, Kiburugwa, Kijichi, Kilungule, Mianzini, Mbagala, Mbagala Kuu na maeneo ya Kongowe Mzinga.

Wizara ilieleza kuwa kata za Toangoma na Mianzini zinahudumiwa na Ofisi za Tanesco  za Wilaya ya Kigamboni na Mkuranga.

Ilieleza jimbo lina wateja 64,501 wanaohudumiwa na njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilomita 1,469.01 kupitia transfoma 301 katika maeneo mbalimbali ya kata hizo.

“Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa shirika na kuimarisha huduma kwa wateja, Jimbo la Mbagala litaendelea kuhudumiwa na ofisi za Tanesco za wilaya za Kigamboni, Mkuranga na Mbagala.

 “Kwa sasa hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Mbagala imezidi kuimarika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha Mbagala cha msongo wa kilovoti 132/33 chenye uwezo wa MVA 50 ambacho kilizinduliwa Februari 22 mwaka 2018,” ilieleza Wizara ya Nishati.

Ilieleza kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme katika maeneo ya Kilimahewa, Changanyikeni, Vikunai Kata ya Toangoma na maeneo ya Mponda, Vigozi, Churuvi Kata ya Mianzini ilikamilika kati ya Oktoba, 2018 na Mei, mwaka jana.

Ilisema kukamilika kwa utekelezaji wa miradi hii kumesaidia kuimarika kwa hali ya upatikanaji umeme katika maeneo ya Jimbo la Mbagala.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles