29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Mbunge ataka mawaziri waungwe mkono

Na MWANDISDHI WETU -DODOMA

MBUNGE wa Kilindi, Omary Kigua (CCM), amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inafanya kazi nzuri licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wabunge wengine wawaunge mkono mawaziri wanaoongoza wizara hiyo kwa kuwa wanafanya kazi zinazoonekana.

Kigua aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

“Kwanza kabisa nawapongeza mawaziri wa wizara hii kwa sababu wanafanya kazi nzuri inayoonekana, na hata Watanzania ni mashahidi kwa sababu wanaona ni kwa kiasi gani ajali na uhalifu zimepungua kwa kiasi kikubwa.

 “Hapo zamani, watu walikuwa wanashuhudia uhalifu unafanyika katikati ya Jiji la Dar es Salaam kama maeneo ya Kariakoo.

 “Lakini kwa sasa umepungua, hivyo ni lazima Jeshi la Polisi lipongezwe katika hilo kwa sababu linafanya kazi nzuri.

 “Pamoja na hayo, naipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa jitihada inazochukua na kuhakikisha inajenga vituo vya polisi pamoja na magereza.

“Najua bado changamoto ni nyingi na ziko kila maeneo, hasa hasa kwa wilaya mpya, lakini namshukuru Waziri kwa kuwa tumepata shilingi milioni 150 kwa ajili ya kujenga nyumba za polisi katika Wilaya ya Kilindi.

 “Pamoja na hayo, bado tuna changamoto ya kupata kituo cha kisasa kwa kuwa wilaya yetu ni ya muda mrefu, yaani tangu mwaka 2002 hakuna kituo hicho.

 “Kwa maana hiyo, namuomba Kangi (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola), aiangalie wilaya yetu ili iwe na kituo cha kisasa cha polisi na vituo vya kata vilivyobaki tutavijenga wenyewe,” alisema.

Alisema katika vitambulisho vya taifa kuna shida kutokana na mchakato huo kwenda taratibu.

 “Na hili linakwenda taratibu, juzi tumepata taarifa kwamba kuanzia Mei Mosi kila mwenye kitambulisho cha taifa ndiyo atakayesajiliwa laini, sasa hili ni tatizo.

 “Ukiangalia mwenyekiti, wizara iliingia mkataba na Kampuni ya Iris Corporation uliosainiwa Septemba, 2014 na mkataba ulikuwa hadi mwaka 2016,” alisema.

Alisema lakini waliongezewa tena mkataba hadi Septemba mwaka jana jambo linalopaswa kufanyiwa kazi na wizara husika.

“Vitambulisho vya taifa ni haki ya kimsingi, ni lazima muongeze kasi ili kuhakikisha kwamba vinapatikana kuanzia ngazi za vijiji hadi mkoa. Nalisema hili maana tunapata malalamiko huko vijijini kwamba bado,” alisema Kigua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles