MBUNGE wa Viti Maalumu, Rebecca Ngodo (Chadema), amelalamikia maji ya wilayani Meru kuwa yanawaharibu meno wakazi wa maeneo hayo.
Akiuliza swali bungeni jana, Ngodo alisema wananchi wa wilaya hiyo wanapata athari za afya ikiwemo kuwa na meno yenye rangi ya kahawia na miguu yenye matege kutokana na maji kuwa na madini ya fluoride iliyozidi.
“Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha watu wake wanapata maji safi na salama kutokana na kodi wanazolipa, Serikali inafanya nini kukabiliana na ongezeko la fluoride katika maji katika eneo hilo,” alihoji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, alisema mikoa iliyoathirika zaidi kwa kuwa na vyanzo vya maji vyenye madini hayo ni pamoja na Kilimanjaro, Singida, Mwanza na Arusha.
“Wizara inaendelea kuhakiki ubora wa maji katika vyanzo vyote vya maji ili kubaini vyanzo vilivyoathirika pamoja na kufanya utafiti wa jinsi ya kupunguza madini ya fluoride katika maji ya kunywa kwa kutumia teknolojia rahisi na gharama nafuu,” alisema Makalla.
Alisema jumla ya vyanzo 121 katika wilaya hiyo vimebainishwa na kuhakikiwa ubora wake na matokeo yameonyesha kuwa asilimia 55 ya vyanzo vya maji vilivyokaguliwa vina kiwango cha chini ya miligramu nne kwa lita moja ya maji inayokubalika kitaifa.
“Wizara kwa kushirikiana na halmashauri husika itaendelea kuhamasisha utumiaji wa vyanzo vyenye madini ya fluoride inayokidhi viwango,” alisema Makalla.