27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge ahoji adhabu kwa wanyanyasaji kijinsia

NA RAMADHAN HASSAN–Dodoma

 MBUNGE wa Viti Maalumu, Anna Gidaya (Chadema), amehoji ni lini Serikali itachukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa wa matukio ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwani  wanadhalilisha utu wa mtoto wa kitanzania.

Akiuliza swali jana bungeni, Gidaya alidai kwamba matukio ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia nchini yameongezeka kwa kiasi kikubwa, hasa ubakaji wa watoto pamoja na kulawitiwa jambo ambalo linaathiri watoto kisaikolojia.

Gidaya alihoji ni lini Serikali itachukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa hawa wanaodhalilisha utu wa mtoto wa kitanzania.

Ikijibu swali hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilieleza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa wanaodhalilisha utu wa mtoto ikiwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti na mimba kwa watoto.

Ilisema imesimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 Kifungu cha 130 (1) 2 (e) ambayo adhabu yake imeainishwa katika Kifungu 131 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambacho kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au kifungo cha maisha kwa yeyote atakayebainika kuwa na mahusiano ya kingono na mwanafunzi.

Aidha, Sheria ya Elimu ya mwaka (1978) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 Kifungu 60 (a) inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu yeyote atakayempa mwanafunzi mimba.

Wizara ilieleza katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 jumla ya mashauri ya unyanyasaji ya watoto 11,270 yalipokewa ambapo 1,431 yalipelekwa mahakamani na kati ya hayo, 974 yalitolewa hukumu.

Ilieleza kuwa Serikali imeanzisha vituo vya mkono kwa mkono (one stop centers) ambapo huduma za matibabu, polisi, sheria na ushauri nasaha hutolewa kwa pamoja.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilieleza hadi kufikia Machi mwaka huu, jumla ya vituo vya mkono kwa mkono 13 vimeanzishwa katika hospitali za Amana, Mwananyamala, Tumbi, Kitete, Sekou Toure, Mbeya FFU, Hai, Shinyanga Manispaa, Kahama Hospital, Mt Meru na Nindo-Iringa. 

Ilisema vituo hivyo vinasaidia katika utoaji huduma kwa waathirika wa ukatili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles