25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe: Nimesikitika Lowassa kuondoka

AGATHA CHARLES

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameelezea kusikitishwa na kitendo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kukihama chama hicho na kurejea CCM.

Mbowe alisema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya mkutano tangu atoke mahabusu katika Gereza la Segerea alipokaa kwa siku 104.

 “Nilisikitika (Lowassa kuondoka Chadema), nikisema nilifurahi nitasema uongo, kwa sababu tulimpokea kwa nia njema. Lakini kwenda kwenye chama kingine cha siasa basi akaseme kweli, sisi tutaendelea kuijenga demokrasia. Na mjadala huu naufungia hapo,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema chama cha siasa kina wajibu wa kujijenga na kuongeza wanachama na kwamba hivyo ndivyo ilivyokuwa katika kumwongeza Lowassa mwaka 2015.

“Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake alisema, chama cha siasa ni dodoki, ukiliweka kwenye maji litanyonya maji, ukiliweka kwenye maziwa litayanyonya maziwa na ukiliweka kwenye maji taka litayanyonya, vyama vya siasa vinavuta watu wa makundi mbalimbali kwa sababu mbalimbali.

“Wako watu wema na wasio wema, wapo wenye kupenda pengine madaraka, wapo watu wanatumwa, wanaendeshwa na wito wa kuwatumikia watu na kuitumikia haki. Kila mmoja katika roho yake ana uelewa binafsi anataka nini kwenye chama cha siasa.

“Japo meza hii tupo Chadema watupu, yawezekana miongoni mwetu tuna ajenda za ziada ambazo hatuzijui, ni mambo ya kibinadamu. Kila mmoja ana malengo, japo tunategemea tunayo yanayofanana, mwisho wa siku lengo tutumie karama zetu kupinga uovu, kuihubiri haki na yaliyo mema na kulaani yasiyo na haki,” alisema Mbowe.

Alisema wapo ambao walianza nao wakashindwa katikati na wengine waliwakuta katikati, wakaenda nao lakini wakashindwa kuendelea.

Alisema kila mmoja ana sababu yake kuwa kwenye chama.

 “Lengo letu ni kuisimamia haki kupitia demokrasia katika nchi, wajibu huo pengine kauona mzito.

 “Unapoona maovu yanafanyika usikemee, unapoona watu wanafungwa bila sababu na usitoe tamko, unapoona watu wanapotea nawe ukayaona ni ya haki, ukakaa kimya, unapoona watu wanapigwa risasi na usiuone uovu, ni bora ukishindwa kulia na sisi, usiwe na sisi,” alisema Mbowe.

LISSU

Alipozungumzia kuhusu mshahara wa Lissu na yanayoendelea kumhusu, Mbowe alisema ni budi wahusika wauvae ubinadamu katika kuamua.

“Hebu tupate aibu kidogo katika maamuzi tunayoyafanya, tuuvae ubinadamu, hao wenye mamlaka wafikirie Lissu awe ni mtoto wao, aliyepigwa risasi zote zile akapona kwa muujiza wa Mungu, ukakataa kumtibu, huyu mtu mnategemea apige magoti alie,” alisema Mbowe.

Alisema anashangaa kuwa wapo wanaosema kama Mtanzania ana shida aje nchini kuyazungumza wakati wao wanapozungumzia hapa wanaishia gerezani.

Mbowe alisema kama kungekuwa na jukwaa la kuzungumza na kuripotiwa kama ilivyo kwenye vyombo vya habari, uhuru wa kusema bungeni na Watanzania waone, wasingehitaji majukwaa ya BBC na CNN au vyombo vingine vya kimataifa.

CUF

Mbowe alisema Chama cha Wananchi (CUF) kinapitia kwenye migogoro mingi ambayo ni ya kutengeneza ikiwa inasababishwa na dhamira ya kudhoofisha upinzani.

“Nawaombea wamalize kinachowezekana salama. Nimemsoma Profesa Ibrahim Lipumba, anatuhukumu sana Chadema namna ambavyo hakukubaliana na Ukawa 2015.  

“Sipendi kubishana na Lipumba, nimtakie heri huko alikoamua kutumikia. Kama kweli anataka kuwatumikia wananchi, tutaona, muda utaongea.

“Haki ya wananchi wa Zanzibar kupitia kwa Maalim Seif (Sharif Hamad) na chama chake, ambayo ilipokwa baada ya uchaguzi 2015, itarejea siku moja, nina hakika. Namwombea mema Seif na timu yake ya uongozi atambue hayo mapito, tunalia wengi kwa pamoja,” alisema Mbowe.

NASSARI

Mbowe alisema suala la aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, kufutiwa ubunge, alilisoma mitandaoni na kwamba huo ndio mchezo wa siasa.

Mbowe alisema hatetei mbunge wa chama chochote kuwa mtoro kwani wabunge kuhudhuria vikao na kamati ni jambo la msingi, lakini ana imani katika maisha ya utawala na uongozi ambako hakuna dhamira mbaya kwani mambo mengine ni ya kiutawala na yanatafutiwa tiba.

Mbowe alisema Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) ni ofisi na ina wasaidizi, alitegemea kwa tukio kubwa kama hilo kungekuwa na taarifa.

“Mimi kama KUB, mbunge wangu anafukuzwa ubunge nasoma kwenye mitandao, hata kuambiana, kwa sababu ya kutokuwepo kwa nia njema.

“Juzi Jumanne, nilikuwa na kikao na Spika (Job Ndugai) Dodoma, baada ya kutoka gerezani nilienda jimboni kuhani misiba kisha Dodoma kwenye ofisi za Bunge.

“Nikamuuliza hali ikoje, kambi ikoje, maana pamoja na tofauti zetu bado lazima tufanye kazi. Jambo hili halikujitokeza naliona mitandaoni jana (juzi) jioni,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema anashangaa inawezekanaje kuwafutia Mbunge wananchi waliopiga kura zaidi ya 100,000 Arumeru Mashariki huku kukiwa tayari msimamizi wa uchaguzi ametangaza kurudia uchaguzi.

Alisema katika uchaguzi huo zinakwenda kutumika zaidi ya Sh bilioni 45 za Watanzania na kwamba hiyo si siasa.

“Nimezungumza na Nassari, nimemwelekeza azungumze na Watanzania. Azungumze na viongozi wa jimbo lake na taifa, aeleze ni nini kimetokea kwa sababu si kweli, kwamba Nassari hajahudhuria vikao vyote vya Bunge na kamati zake,” alisema Mbowe.

Alisema fedha nyingi zinatumika kurudia uchaguzi hata kwa sababu ambazo si muhimu.

“Kama Spika na timu yake itaendelea kufanya hayo ni bahati mbaya kwa taifa,” alisema Mbowe.

KUKUTANA NA JPM

Wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari likiwamo la kuomba kukaa na kuzungumza na Rais Magufuli, Mbowe alisema:

“Chadema tumekuwa wazi siku zote wala hatujawahi kuwa na shida ya kuonana na kiongozi yeyote wa nchi hii akiwamo Rais.

“Hatujawahi kuwa na shida ya kukaa na Rais. Ila kuonana na Rais hulazimishi, lazima aridhie yeye. Lakini sisi kama Chadema hatujakataa kukaa na Rais, mimi sina ugomvi na Rais mwenyewe, hatuna chuki binafsi, tunakosana katika misingi ya uendeshaji wa nchi na uminywaji wa demokrasia.

“Lakini hata kule Spika ambaye anaminya wabunge wa upinzani, naonana naye, ndio uendeshaji wa taasisi, hatuna migogoro binafsi,” alisema Mbowe.

MAHABUSU

Akizungumzia uwepo wao pamoja na Mbunge Ester Matiko gerezani, Mbowe alitaja maeneo sita ambayo aliyabaini huko.

Alisema kupelekwa kwao gerezani kulitokana na mfumo wa kile alichokiita utatu haramu aliosema ni kati ya hakimu, waendesha mashtaka/DPP na mamlaka isiyojulikana.

Alisema anaishukuru Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu kwa uamuzi wao uliowafanya kuwa nje kwa dhamana baada ya siku 104.

Mbowe alisema hajutii kuwa gerezani kwa siku hizo kwani kulimwezesha kuandika kitabu hivyo atatoa machapisho ya alichokiona.

Kutokana na aliyoyashuhudia Mbowe, aliomba mamlaka, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Kamishna wa Magereza, kufanya operesheni maalumu ya miezi mitatu ya mkakati wa kuondoa nusu ya mahabusu wanaooza gerezani.

Alisema neno ‘upelelezi unaendelea’ limekuwa likitumika kama mwavuli kuficha madhaifu ya upelelezi hivyo muda wa upelelezi udhibitiwe.

Jambo lingine ambalo Mbowe alitaka lishughulikiwe na mamlaka hizo ni tabia ya kuwafikisha mahabusu watu wasio na hatia na hivyo kusababisha msongamano.

Alisema jambo hilo linawaharibu wale ambao hawana hatia.

“Gereza la Segerea pekee kuna mahabusu kati ya 2,300-2,450, lakini uwezo wa gereza hilo ni mahabusu 750. Watu wanalala kitu kinaitwa mchongoma yaani mnalala kwa ubavu mmoja kwa masaa matatu, nyapara anapiga kibao kisha mnageuka upande mwingine,” alisema Mbowe.

Alisema wana imani na mfumo wa mahakama lakini zipo nyingine zinahitaji jicho la ziada ikiwamo mahakama za mwanzo.

Alisema asilimia 60 ya mahabusu wa Gereza la Segerea wanatokea mahakama za mwanzo ambako hakuna mwanasheria anayewatetea huko.

 “Tukiondoa asilimia 50 ina maana magereza yatapunguza watu na kesi zitakwenda mbio,” alisema Mbowe.

Alisema suala jingine lililomsikitisha ni askari wa magereza kujinunulia sare za kazi wenyewe.

“Nikawauliza askari magereza inawezekanaje, wakasema kwa zaidi ya miaka minne, tano hatujawahi kupewa sare na magereza. Kwa hiyo unakuta mjanjamjanja anavaa vizuri ambaye amechokachoka unaona amechoka kweli kuanzia kiatu hadi kila kitu. Askari hao ni nusu wafungwa, wapatiwe bajeti ya kutosha, wanafanya kazi ngumu,” alisema Mbowe.

Kitu cha nne ambacho Mbowe alikiona ambacho alitaka kifanyiwe kazi katika operesheni safisha magereza ni ugonjwa unaoitwa burudani ambao uko magerezani.

Alisema huo ni ugonjwa wa ngozi ambao chanzo chake ni kunguni na chawa ambao wanasababishwa na uchafu.

Alisema ikifanyika operesheni hiyo ugonjwa huo utaisha magerezani kwani ukiachwa kwa muda mrefu unaathiri baadhi ya ogani.

Alisema kutokana na msongamano wapo ambao hushindwa kuoga zaidi ya wiki, hivyo wanaambukizana ugonjwa huo kutokana na kulala watu watatu katika godoro dogo moja.

MATIKO

Awali, Matiko, alitaja mambo tisa aliyoyabaini akiwa gerezani Segerea.

Alisema baadhi ya wanawake wanaokamatwa wanadhalilishwa wakiwa vituo vya polisi kwa kubakwa.

Gazeti hili lilitaka kujua iwapo Mbunge huyo tayari ana majina ya askari wanaohusika pamoja na hatua atakazochukua ambako alijibu kuwa suala hilo atakwenda kupaza sauti bungeni.

Matiko pia alisema kuna msongamano mkubwa wa mahabusu na wafungwa katika gereza hilo la wanawake alilokuwapo ambao uwiano wa wafungwa na mahabusu ni nne kwa moja na kwamba mahabusu wanaweza kuwa 250 lakini wafungwa ni 50.

Alisema hayo yote yanasababishwa na ucheleweshwaji wa kesi hivyo alishauri hilo lifanyiwe kazi na bunge.

Alisema pia kuna ombaomba wengi wanaokamatwa wakiwa na watoto wadogo ambako Mbunge huyo alisema jambo hilo linapaswa kutatuliwa na si kupelekwa gerezani.

Matiko alizungumzia pia mahabusu kuchanganywa na watu wenye matatizo ya akili ambako alidai huko walikuwa na wagonjwa wawili ambao walifikia hatua ya kufanya fujo.

Jambo la tano alilozungumzia Matiko ni mahabusu kukaa muda mrefu na hivyo Serikali kuingia gharama.

Katika suala la sita alisema, hakukuwa na gari ya wagonjwa katika gereza hilo na kwamba wagonjwa walibebwa kwenye gari aina ya pick up ambako hakuna sehemu ya kutundika drip.

Suala la saba alisema pia kuna uhaba wa magari ya kuwapeleka mahabusu mahakamani na hivyo kesi nyingi zinachelewa.

Alisema jambo la nane ambalo aliliona na linatakiwa kufanyiwa marekebisho ni ofisi ya DPP kutumia vibaya kifungu cha 2 2 5.

“Unakuta mahabusu amekaa miaka mitatu, anaachiwa kisha anakamatwa tena, mahakimu wanakataa kumpokea lakini unakuta polisi wanaenda kukaa naye kituoni. Kesi hizo ninazo mbili raia amekaa kituoni zaidi ya miezi tisa, nje ya miaka mitatu, minne aliyokaa Segerea. Anapewa kesi nyingine, nikasema hili ni jambo la kuangaliwa wabunge wenzangu wananisikia, lifanyiwe marekebisho,” alisema Matiko.

Alisema jambo lingine alilobaini ni mtu kukamatwa kwa kosa la mtu mwingine pale wanapomkosa mhusika.

MAGEREZA WAJIBU

Kutokana na madai hayo, MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini (SP), Amina Kavirondo, ambaye alikiri kuwapo kwa changamoto ya idadi kubwa ya mahabusu magerezani.

AS Kavirondo, alisema magereza haina idadi kubwa ya wafungwa, lakini changamoto ipo kwa mahabusu na kwamba suala hilo si la kuzungumzwa na magereza pekee bali idara tatu au nne ambazo zinahusika na mambo ya haki jinai.

“Mbowe anaposema kuna msongamano  magerezani, alikuwa anamaanisha nini, wafungwa au mahabusu? Kama wafungwa sisi magereza hatuna changamoto hiyo, lakini kama ni mahabusu ni kweli na ukiniuliza sababu idara ya magereza pekee haitakuwa na jibu kwa sababu ngazi hiyo inahusisha idara mbalimbali za haki jinai,” alisema AS Kavirondo.

Akizungumzia madai ya uchafu, AS Kavirondo, alihoji kwamba Mbowe anazungumzia usafi kwa kulinganisha na nini?

“Kama kuna msongamano wa mahabusu, hiyo hali ya usafi anataka kuilinganisha na nyumbani kwake au wapi? Hata hiyo shida ya maji anayodai analinganisha na wapi?” alihoji.

Akizungumzia hoja ya Matiko ambaye alisema watu wenye matatizo ya akili wanachanganywa na wafungwa wenye akili timamu, AS Kavirondo, alihoji kama Matiko ni daktari na ana vielelezo vya kitabibu vinavyoonyesha kuwapo watu wenye matatizo ya akili wamechanganywa na mahabusu.

Alisema Jeshi la Magereza lina idara ya afya na kuna taratibu zinazofuatwa, hivyo kwa mtu mwenye tatizo lolote la kiafya, jeshi hilo hutumia taratibu zake kumtibu, kupanga sehemu gani sahihi ya kumhifadhi.

“Matiko si daktari na hana haki yoyote ya kisheria kuzungumzia afya ya mtu. Sisi ndio tunaohifadhi watu, tunayajua mengi ya magerezani kuliko yeye.

“Nimesikia wamedai kuwa hali ya uchafu watu wana ukurutu, tuwaulize wao wana ukurutu? Waache kupotosha umma,” alisema AS Kavirondo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles