NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ametangaza rasmi kutetea nafasi yake baada ya kuombwa kufanya hivyo na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Pamoja na hilo, pia amewakaribisha wanachama wa Chadema wanaohisi wana uwezo wa kushinda nafasi hiyo kujipima kwake.
Alitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuchukuliwa fomu na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mkoa wa Kigoma, Yasin Mzigo, kwa niaba ya viongozi wengine wa mabaraza ya wazee alioambatana nao kutoka mikoa mbalimbali.
Baada ya Mbowe kupokea fomu hiyo ya kukubali kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kutetea kiti chake, aliwashukuru wazee hao na kueleza sababu ya kukubali ombi lao la kumtaka awanie tena nafasi hiyo ya juu ndani ya Chadema.
“Kuna mambo mawili yananipa wakati mgumu kukubali ombi hilo, kwanza Chadema ni chama kilichosheheni watu wenye taaluma, uzoefu na weledi mbalimbali, kwanini iwe mimi. La pili ni namna makundi mbalimbali yalivyojitokeza kutaka niwanie uenyekiti hali inayoweza kutoa nafasi kwa wapenda majungu kufikiria kwamba jambo hilo nimelipanga mimi,” alisema.
Alisema awali hakukusudia kugombea nafasi hiyo na ndiyo maana aliwahi kutoa kauli ya kukataa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho mbele ya kikao cha Kamati Kuu, ambapo aliwataka wanachama kumchagua mtu mwingine akiongoze chama.
“Niliwaeleza kwamba nahitaji nimpate Mnyamwezi mwingine ili nimkabidhi jiwe hili, lakini Kamati Kuu ilikataa na ikatoka na tamko la kukataa kuachia uenyekiti, ingawa niliwaambia kwamba naacha nafasi hii si kwa sababu naichukia Chadema na sio kwa sababu namwogopa mtu yeyote, lakini ni kwa sababu nimekitumikia chama hiki kwa umri wangu wote na kwa uadilifu.
“Na mimi ni binadamu, nina familia na maisha mengine, hivyo nahitaji niendelee na maisha mengine, lakini kauli za viongozi wengine na makundi mbalimbali zimekuwa za kunitaka kukubali wito wa kuchukua tena fomu, ni kweli hadi sasa sijachukua fomu na kesho natarajia niondoke asubuhi kwenda Uingereza na ninawashukuru wote walioona naweza kuongoza tena chama hiki,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alimweleza mwakilishi huyo wa wazee ambaye ndiye aliyemchukulia fomu kwa niaba ya wanachama wengine wa Mkoa wa Kigoma kuwa akiwa mpiganaji, amejikuta akipata wakati mgumu kutokana na misimamo yake ya kupigania haki ya kutetea demokrasia, lakini katu hatorudi nyuma kwa masilahi ya taifa.
Alisema kuwa katika maisha yake ndani ya Chadema, hajawahi kuomba kuwania nafasi ya uenyekiti na badala yake amekuwa akiombwa kuwania nafasi hiyo na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Akitolea mfano mwaka 2004, Mbowe alisema nafasi hiyo aliombwa kuwania na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema marehemu, Bob Makani, ambaye alikuwa anamaliza muda wake wa uongozi ndani ya chama hicho.
Pamoja na kutakiwa kufanya hivyo, alisema alikataa kutokana na kubanwa na shughuli zake hali iliyofanya Bob Makani kuunda jopo la wazee ambao walimchukulia fomu na kumtaka kujaza, akakubali kugombea.
Alisema mwaka 2005 wakamuomba tena kugombea baada ya mgombea aliyekuwa amepitishwa kuwania nafasi hiyo na chama, Profesa Mwesiga Baregu kujitoa dakika za mwisho.
Mbowe alisema kuwa hata mwaka 2009 aliombwa tena kuwania uenyekiti akagoma, lakini wazee wa Dar es Salaam walimuomba tena, ikiwamo na kumjazia fomu, lakini kwa mwaka huu imekuwa tofauti kwani fomu amechukuliwa na wazee kutoka Kigoma.
Alitoa wito kwa wale wanaofikiria kwamba alitengeneza jambo hilo kwa kusema: “Hata ninyi kama kuna mwandishi wa habari ana nia ya kuvuta fomu avute tu, aone ngoma itakavyokuwa na anayetaka kujipima aje apime, nawahakikishia hii ngoma nitaicheza tena na anayefikiria ana ubavu wa kucheza ngoma hii ajitokeze,” alisema.
Mbowe alisema kuwa kuna changamoto nyingi za kuendesha chama cha siasa na wala hakuna raha kama inavyokuwa inafikiriwa na wengi.
“Ndugu zangu kazi ya kuongoza na kujenga chama cha siasa si mchezo, ni kazi inayohitaji ‘commitment’ na si kazi ya ulaji kama wengi wanavyofikiri kwamba Mbowe anatafuna ruzuku… ipi? Kazi hiyo ni ya hatari kwani inakulazimisha wakati wote kutoonana na watoto wako, na unaweza kuondoa maisha yako wakati wowote kama usipoifanya kwa uaminifu na ujasiri, kwani hakuna jeshi wala silaha itakayosaidia,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo kazi hiyo itafanyika kwa uhakika, hata uadilifu na ulinzi wa Mungu utaupata kwa uhakika.
“Nimefanya kazi yangu kwa kujiamini sana, sina hofu ya usalama wa jeshi, polisi au raia ninamuheshimu mdogo hadi mkubwa, mwenye mamlaka na asiyekuwa nayo, lakini kamwe simwogopi yeyote, nadhani naweza kusema hiyo ndiyo imekuwa silaha iliyoniwezesha kukifikisha Chadema hapa kilipofika,” alisema.
Mbowe aliongeza kuwa kazi ya kukiimarisha chama kwa miaka 20 ameifanya kwa kushirikiana na wapambanaji wengine, lakini wapo aliowaacha njiani kwa kutokujua na wengine kwa kutumika huku wengine wakipotea kwa kuishiwa nguvu.
“Wapo waliofanikiwa kujenga umashuhuri kwa kupitia chama hiki na kupata senti mbili tatu, basi wanaona malengo yao yametimia, lakini yangu na wengine ni kuhakikisha taifa hili linapata viongozi waadilifu wenye kuwajali wananchi wote wakiwamo maskini,” alisema.
Akizungumzia viongozi wanaojiuzulu nyadhifa zao katika chama hicho, Mbowe alisema kuondoka kwao kumechangiwa na kukimbia mbinu mpya zilizobadilishwa na chama hicho za viongozi wa juu kuchaguliwa na wanachama.
Alisema sababu hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kwa sasa chama hicho kuwa tofauti na vingine, kutokana na kuanza kuwajengea hamasa wananchi.
Mbowe alikimwagia sifa Chadema kwa kusema kuwa amekijenga kwa weledi na kukifanya kuwa tofauti na kilivyokuwa hapo nyuma ambako viongozi wa mikoani walikuwa wakipeana nafasi.
“Nikifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama hiki, naamini nitakuwa nimekwenda kukiongoza chama ambacho kina mtandao ambao haujawahi kutokea katika chama chochote cha siasa nchini,” alisema.
Kuhusu kauli za kubomoka kwa Chadema, Mbowe alipinga na kusema kwa sasa chama hicho kipo imara na ukweli huo utathibitishwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu ujao.
“Watauelewa muziki wa Chadema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuona namna tulivyojenga mtandao wa chama na oganaizesheni, sisi hatujengi majengo bali tunajenga fikra za watu nchi nzima, kwani kazi ya kujenga ofisi si kazi ya chama hiki, kwani kipaumbele ni kujenga fikra za wananchi kudai haki zao na wale wanaosema dhaifu hawaielewi Chadema,” alisema.
Mbowe aliongeza kuwa Chadema mpya itaonekana Septemba 14, 2014 kutakapofanyika mkutano mkuu wake ambako watapata fursa ya kuonyesha mwendo wa chama hicho.
“Nawashukuru viongozi wangu wakuu bila kujua wamepanga tarehe ya mkutano huo siku niliyozaliwa, lakini sikubatizwa hadi siku ya Uhuru Desemba 12, 1961, viongozi wa Chadema wamepanga kufanyika mkutano mkuu siku ya sherehe ya kuzaliwa kwangu na wale wanaoiombea ajali Chadema hawatafanikiwa,” alisema.
Julai 2, mwaka huu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia kwa Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, ilitoa taarifa na kusema kuwa Mbowe hana sifa za kugombea uongozi wa chama hicho, kwa vile Katiba ya chama hicho ya mwaka 2006 inambana.
Nyahoza alisema Katiba ya Chadema ya mwaka 2004 ilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka kilichoeleza kuwa kiongozi aliyeongoza vipindi viwili vya miaka mitano mitano hawezi kuwania tena nafasi hiyo.
Mvutano huo ulikifanya chama hicho kumlaumu Msajili, Jaji Mutungi, kikidai ofisi yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.
Julai mosi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema Jaji Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za viongozi wa chama hicho, bali wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama hicho pekee.
Mnyika alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema haikurekebishwa bali iliundwa upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa chama na kwamba Agosti 13, 2006 ilizinduliwa na nyaraka zote alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa wakati huo, John Tendwa.
Kiukweli kamanda mbowe we ndio star wa chadema yetu ila fanya utaratibu wa kuwa television ya chadema ili tusitishiwe na hivi vituo binafsi kwa habari za chama