24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE, LOWASSA WAWASHA MOTO MONDULI


ABRAHAMU GWANDU Na ELIYA MBONEA-MONDULI

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana walihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Monduli ikiwa ni lala salama ya kampeni za ubunge katika jimbo hilo, kabla ya uchaguzi keshokutwa.

Akizungumza kwenye mkutano huo ikiwa ni mkutano wake wa kwanza tangu wakati wa kampeni za mwaka 2015,  Mbowe aliwashukuru wananchi hao kwa kumpa Lowassa kura nyingi wakati wa uchaguzi mkuu.

“Lowassa alipata kura za kutosha kuwa Rais, lakini Tume ya Uchaguzi (NEC) ilimtangazia kura milioni 6.8 wakati Rais John Magufuli akipata kura zaidi ya milioni 8. Monduli mlitupa Rais wa mioyo ya watu aliyekubalika nchi nzima mlipiga kura za kutosha.

“Mlitupa wabunge na madiwani kabla ya hapo tulikuwa na madiwani 404 lakini baada ya uchaguzi mwaka 2015 tulipata madiwani 1,180, wabunge walikuwa 42  mkatupa 115, hii ni kazi kubwa mliyoifanya wana Monduli na Watanzania,” alisema.

Mbowe alisema shida ya Watanzania wakati huu si kununua ndege wala kujenga reli za kisasa kwa sababu yote yanaweza kufanyika lakini kama wananchi hawana uhuru na haki, yote hayo yatakuwa hayana maana.

“Wabunge, madiwani wananunuliwa leo ili wahamie CCM, hii yote ni kuwanyima uhuru na haki wananchi waliowachagua kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 kwa sababu  ilikuwa haki yao kuwapigia kura wanaonunulia leo.

Mbowe alimtaka Rais John Magufuli na viongozi wenzake kutengeneza Tanzania ya ushindani wa hoja na si vitisho kwa sababu  msingi wa kwanza katika taifa lolote ni haki.

“Huwezi kuzungumza kuna amani na uhuru wakati wakuu wa wilaya wanakamata viongozi wa upinzani na watu wengine wanawaweka ndani bila sababu za msingi, ndugu zangu hakuna kiongozi aliye juu ya sheria.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama hicho wakiwamo wabunge,   Mbowe alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa uchaguzi mdogo unaofanyika ni uchafu wa siasa.

“Uchaguzi huu ni msingi wa kuchezea haki na uhuru wa wananchi, haiwezekani tutumie zaidi ya Sh bilioni tano kwenye jimbo moja kwa ajili ya kurudia uchaguzi wa  watu walionunuliwa.

Awali, Lowassa akizungumza kwenye mkutano huo, alisema ujinga wa kurudia uchaguzi umekuwa ukimsumbua mara kwa mara na hivyo kuona haja kubwa ya kuwapo   Katiba mpya.

“Kuna wajinga wanasema eti Monduli hakuna maji, ndiyo maana wamehama chama na kusababisha hasara hii kubwa  kwa wananchi walipa kodi.

“Nilipokuwa Waziri wa Maji, nilichaguliwa na Rais (Benjamin) Mkapa  kuongoza wizara hiyo, nilihangaika kufanya mazungumzo na Benki ya Afrika (ADB) ambao mwisho walitupatia mkopo wa kuchimba visima vikubwa vya maji eneo la Ngaramotoni.

“Leo hii Monduli kuna maji ya kutosha, hawa viongozi wa Serikali wanafanya uzembe kulipa bill za umeme halafu wanakuja mbele yenu kudanganya eti Monduli hakuna maji, waongo wakubwa hawa.

“Nawaomba wananchi wa Monduli mnipe heshima kwa kuhakikisha Kalanga hapati hata kura moja, nitakuwa hapa Jumapili kuhakikisha Laizer anachaguliwa,” alisema Lowassa.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godless Lema, aliwaambia wananchi hao kama wakiona mwanaume anakuwa na bei basi huyo si riziki mbele ya jamii.

“Niwaombe, lindeni kura zenu ili mumpe heshima Laigwanan Lowassa hapa Monduli,” alisema Lema.

Naye Fred Lowassa, aliwataka wananchi wa Monduli kumchagua Laizer kwa sababu  atawafaa katika suala zima la kuwaleta maendeleo.

Akihitimisha mkitano huo, Mgombea ubunge Laizer, aliwaomba wamchague ili akashughulikie suala zima la ankara za maji zilizowashinda viongozi wa serikali  na masuala mengine yakiwamo ya migogoro ya ardhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles