MBOWE KUHUDHURIA KUAPISHWA RAIS MPYA GHANA

mbowe

Na Tobias Nsungwe

MWENYEKITI wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, ni miongoni mwa wageni mashuhuri walioalikwa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo na Makamu wake, Dk. Alhaji Mahamudu Bawumia.

Sherehe za kuapishwa rais huyo zinatarajiwa kufanyika leo jijini Accra.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema makao makuu, Mbowe na ujumbe wake waliondoka nchini jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao pia wanatarajiwa kushuhudia kuapishwa kwa Spika wa Bunge la Ghana. Pia wataona wabunge 275 waliopatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana wakila kiapo.

Taarifa ya Chadema pia ilisema Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Mashinji, watapata fursa ya kufanya mazungumzo na Rais Akufo-Addo yanayotarajiwa kufanyika kesho.

Mbowe pia atapata nafasi ya kula chakula cha mchana na rais huyo mpya aliyetoka chama cha upinzani.

“Kabla ya hapo, mapema asubuhi ya siku hiyo, viongozi wakuu wa Chadema watakuwa sehemu ya msafara utakaomsindikiza Rais Nana Akufo-Addo, kwenda kwenye ibada ya asubuhi, itakayofanyika eneo la Kyebi, kisha jioni msafara utarejea jijini Accra kuendelea na ratiba nyingine,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa pia ilisema ziara ya Mbowe nchini Ghana ni mwendelezo wa urafiki na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu sasa kati ya Chama cha Rais Nana Akufo-Addo cha New Patriotic Party (NPP) pamoja na Chadema, tangu vilipokutanishwa kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) na ule wa Afrika (DUA).

Viongozi wengine mashuhuri kutoka Afrika walioalikwa katika sherehe hizo ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC), Kizza Besigye, kutoka Uganda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here