25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE AELEZA MIKAKATI YA CHADEMA

NA OSCAR ASSENGA-MUHEZA


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema malengo makubwa ya chama hicho ni kujiimarisha kanda ya kaskazini, hasa Mkoa wa Tanga, kutokana na kutokufanya vizuri katika uchaguzi mkuu uliopita uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Mbowe, ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, aliyasema juzi, wakati wa ziara yake wilayani Muheza ya kuangalia uhai wa chama na kufungua matawi ya wakereketwa na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2019.

Mbowe alisema Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa ambayo chama hicho hakikufanya vizuri katika chaguzi zilizopita, hivyo kulazimika viongozi waandamizi wa chama hicho wagawane majukumu ya kufanya ziara katika wilaya zote, ili kuweza kuona namna gani ya kujiimarisha.

Alisema lengo la chama hicho baada ya kumalizika uchaguzi mkuu lilikuwa kuzunguka nchi nzima, kabla ya kuzuiliwa na Serikali ili kutoa shukrani kwa wananchi kwa kupiga kura nyingi kwa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya wananchi, Ukawa, Edward Lowassa.

Aliongeza kuwa, muda huu watauangalia Mkoa wa Tanga ambao bado unaonekana kuwa ni ngome ya CCM kwa kuweka mazingira mazuri ya kuivunja ngome ili kuhamasisha  wananchi wake kufanya mabadiliko ya makubwa kwenye chaguzi zijazo

“Tuna malengo mazuri ya kutaka kujua hali ya kisiasa hapa nchini, uhai wa chama chetu katika kila eneo la nchi hii. Hali ya kiuchumi na kufanya hivi ni miongoni mwa majukumu yetu tukiwa kama viongozi wa kisiasa,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema, chama hicho kimeamua kujikita kwa siku sita katika kanda ya kaskazini ili kupanda mizizi, ikiwa sambamba na kufungua matawi na ofisi za wilaya, ikiwa ni maandalizi ya awali kwa uhai wa chama hicho katika kanda hiyo.

Naye Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema),  alisema wananchi na wanachama kwa ujumla wanapaswa kuanza kujipanga mapema ili kuweza kukabiliana na CCM 2020.

“Hakuna sababu ya kuogopa, mapambano ya kisiasa ni magumu na yanahitaji ukomavu wa hali ya juu, hivyo ndugu zangu lazima mjitoe kwa hali na mali ili tuweze kupata ukombozi wa kweli,” alisema Silinde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles