22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

MBOTO ATAJA KIRUSI HATARI BONGO MUVI  

MbotoNA KYALAA SEHEYE HANCHA

KAMA ni kipaji amejaliwa na anajua kikitumia vyema. Haji Salim maarufu kama Mboto ni mchekeshaji mkubwa hapa Bongo aliyefanikiwa kuiteka hadhira yake. Ubunifu wake ni kati ya silaha zinazomfanya akubalike zaidi.

Nje ya kamera, Mboto hana maringo, ni msikivu na mpole wa kiasi lakini ukiwa naye karibu andaa mbavu zako, maana vituko vyake vinaweza kuchanachana mbavu zako.

Komediani huyu kiraka ambaye amepata kucheza sinema nyingi kwa kushirikiana na mastaa wengine wa filamu Bongo kama Aunt Ezekiel na Irene Paul, ni mwongozaji mkali ambaye ameshawaongoza mastaa wakubwa wanaokubalika hapa Bongo.

Kati ya mastaa ambao alipata kuwaongoza katika sinema mbalimbali ni pamoja na marehemu Adam Kuambiana, Jacob Stephen ‘JB’, Salome Ndumbangwe Misayo ‘Thea’, Hashim Kambi na wengine wengi.

Ni sahihi zaidi kusema kuwa Mboto anajua kutumia vyema karama zake na kuzitofautisha. Utakapomkuta akiwa nyuma ya kamera akiigiza atakuwa tofauti kabisa na pale ambapo utamkuta pembeni ya wasanii walioko mbele yake akiwaongoza kuhakikisha anapata kitu kizuri.

Diva wa sinema nchini, Irene Paul aliwahi kusema kuwa, alipata wakati mgumu sana wakati walipokuwa location wakirekodi Filamu ya Kibajaj kutokana na namna Mboto alivyokuwa akiwavunja mbavu karibu muda wote walipokuwa katika kazi hiyo.

Mbali na Kibajaj, Mboto amecheza sinema nyingine kama Nampenda Mke Wangu, Bana Kongo, na Kitanzi. Nje ya uigizaji, Mboto ana mkataba na kampuni inayodili na kuibua vipaji vya wasanii wa filamu nchini iitwayo Tanzania Movie Talent ‘TMT’ akiwa kama mtangazaji wa shoo hiyo.

Hapa chini ni sehemu ya mahojiano kati ya polisi wa Swaggaz na Mboto. Fuatilia…

My Style: Vipi kuhusu maisha yako ya kiuhusiano? Umeoa au una mchumba?

Mboto: Sijaoa ila nina mtoto mmoja wa kike na mchumba ni majaaliwa ya Mungu,  namuomba Mungu sana, kwa kuwa ninapenda mke wangu awe mcha Mungu, hiyo ndiyo siri yangu kubwa kuhusu mwanamke wa ndoto zangu.

My Style:  Mboto ni mtu wa aina gani nje ya sanaa?

Mboto: Ni mcheshi na mpenda amani, kwa kifupi sijabadilika sana, ukiniudhi ndiyo nakasirika lakini usiponiudhi utafurahi. Yaani mimi kila ninayekaa naye karibu lazima acheke… napenda kuwachekesha watu ili kuweka akili ya mtu sawa, siyo mnaongea serious tu muda wote, kichwa kinaweza kumuuma.

My Style: Unapenda kuishi vipi?

Mboto: Napenda sana amani na utulivu ila ukileta mbwai mbwai tu, huwa siangalii hilo kama ukorofi hata mimi nauweza ila mstaarabu sana, zaidi ya saana.

My Style: Ustaa una faida gani kwako?

Mboto: Faida zipo nyingi, kuna baadhi ya huduma napata bila tabu, hiyo yote ni kutokana na kujulikana. Mfano hata ukiingia sehemu fulani, Mboto kaingia. Napata heshima yangu kama msanii ambaye natoa mchango kwa jamii.

My Style: Zipo hasara labda ambazo unazipata kutokana na ustaa wako?

Mboto: Kiukweli sina hasara na ustaa wangu, kwa kuwa mimi siyo mtu wa skendo wala mashauzi. Hata nikitaka kwenda kununua kitu Tandale, huwa nakwenda bila presha. Sina kawaida ya kumuogopa mtu na ninafurahia mashabiki wangu kunifuata, kwangu siyo usumbufu kwa kuwa ndiyo najua kazi yangu inapendwa kiasi gani.

My Style: Kwa upande wa siasa, unashabikia chama gani?

Mboto: Mimi sina chama, bali namkubali mtu kwa sera zake. Kama utendaji kazi wa Rais Magufuli naukubali kabla hajawa Rais na hata sasa anaendelea kufanya vizuri.

Wapo watendaji ambao nawapenda, naona mtu hapa anafanya kazi, tusiangalie sura ya mtu au utajiri wa mtu tuangalie utendaji wake, atatusaidia vipi kujikwamua katika maisha. Ndiyo sera yangu hiyo dada.

My Style: Unachukizwa na vitu gani?

Mboto: Nachukia sana majungu, kutukanana kisa mwenzio amepata mafanikio, team zisizo na maana… bora ziwe team za kuongeza kipato, unafiki tu. Mtu anapofanya kitu kizuri tushirikiane na kupeana sapoti, siyo unafiki.

Ukweli ni kwamba wasanii wengi ni wanafiki ndiyo maana wanavuma kidogo na kupotea, lakini kama uko kiroho safi huwezi kupotea kwenye tasnia. Hiki ni kirusi hatari sana kinachoua sanaa yetu ya filamu. Wasanii tupendane, tuache team zisizo na maana.

My Style: Mwisho kabisa, una ushauri gani kwa wasanii wenzako?

Mboto: Ushauri wangu jamani wasanii tufanye kazi, tusipende kuendekeza majungu na kudharau wengine. Usijione staa kuliko mwingine, kila mtu katika sanaa kipo ambacho anajua zaidi yako, ipo siku utamuhitaji, sasa kama ukiwa umeshamwonyesha dharau na majungu, bila shaka utakosa msaada wa mwenzako. Kifupi nahubiri upendo na ushirikiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles