29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mbio za Kilimanjaro Marathon 2022 zazinduliwa

Safina Sarwatt, Kilimanjaro

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 zimezinduliwa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni takribani mwezi mmoja kabla ya kufanyika mbio hizo na ambazo zinasubiriwa kwa hamu kubwa.

Hafla hiyo iliyowakutanisha wadau mbalimbali, iliandaliwa na Hoteli ya Kibo Palace – kampuni ambayo ni moja ya wadhamini wenza wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai(pichani) amewapongeza wadhamini na waandaaji wa mashindano hayo kwa kuhakikisha mbio hizo muhimu katika kukuza sekta ya michezo na uchumi na ambazo zimekuwa kivutio kwa wadau wengi wa michezo yanakuweko kwa miaka 20 sasa.

Wadhamini katika hafla ya maadhimisho haya ya miaka 20 ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu) Tigo (21km) na Grand Malt (5km).

Wadhamini wa meza za maji ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement na Kilimanjaro Water. Wasambazaji rasmi ni GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles na Surveyed Plots Company Ltd (SPC).

“Hili ni tukio kubwa ambalo linaunufaisha Mkoa ya Kilimanjaro, Mikoa jirani na Taifa kwa ujumla kwani kuna fedha nyingi za kigeni zinazopatikana kutokana na shughuli wanazofanya wageni wanaokuja nchini kabla na baada ya mbio za marathon,” amesema Mkuu wa Mkoa.

Amesema serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na waandaaji na wadhamini wa mbio hizo ili kuhakikisha tukio hili linaendelea kukua lengo kuu likiwa ni kuboresha utalii kupitia michezo hapa nchini, ambapo alitoa wito kwa wadau wengine wa michezo kuiga kazi nzuri zinazofanywa na wandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon.

“Tunawashukuru kwa jinsi mlivyojipanga sana kwani hii inatupa wakati rahisi kama Serikali kutoa ushirikiano wetu kutokana na ukweli ya kuwa mmejipanga vyema huku mkiishirikisha Serikali ya Mkoa; hili linatuweka katika nafasi nzuri na rahisi zaidi katika kuhakikisha kuna usalama wa uhakika kabla na baada ya mbio za Kilimanjaro Marathoni,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi, ambaye pia ni Meneja wa Chapa ya Grand Malt, amesema maadhimisho ya 20 ya mbio za Kilimanjaro marathon ni mafanikio makubwa haswa ikitiliwa maanani ya kuwa Kilimanjaro premium lager imekuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo tangu kuasisiwa kwake miaka 20 iliyopita.

Amesema wao kama wadhamini wakuu wamejipanga vyema kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 20 ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon ambayo yatahusisha matukio ya kusisimua katika wiki nzima ya kuelekea mbio hizo ambapo alisema jumla ya shilingi milioni zimetengwa kwa ajili zawadi.

Irene meongeza kuwa washindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake kwa mbio za kilomita 42 watazawadiwa Sh milioni 4 kila mmoja na kwamba Mtanzania mwanamume au mwanamke atakaeshika nafasi ya kwanza katika mbio za kilomita 42 atapata zawadi ya ziada ambayo alisema ni motisha ya Sh milioni 1.5 kila mmoja.

Aidha, ametoa wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizo kuhakikisha wanajiandikisha mapema kupitia mtandano wa www.kilimanjaromarathon.com na kupitia TigoPesa kwa kupiga 14920#.

Irene pia alitoa wito kwa washiriki wa mbio za 5km (Mbio za kujifurahisha) ili kuepuka kukosa fursa hiyo pale namba zitakapokwisha kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo amewapongeza waratibu wa mbio hizo kwa mafanikio waliyopata kwa miaka 20 sasa, ambapo ametoa wito kwa wale wanaotarajia kushiriki mbio hizo kutumia mtandao wa Tigo Pesa kujiandikisha kwani jambo hilo limerahisisha mchakato mzima kujiandikisha kwa ajili ya ushiriki wa mbio hizo.

“Sisi tukiwa ni wadhamini wa mbio za kilomita 21, maarufu kama Tigo Kili-Half marathon kwa zaidi ya miaka 7 sasa, tunatarajia mbio za mwaka huu zitakuwa ni za kusisimua, ambapo tunatarajia washiriki zaidi ya 5,000 kutoka ukanda mzima wa Bara la Afrika kutokana na kuongezwa kwa thamani ya zawadi za washindi,”amesema Kinabo.

Kwa upande wao, Waandaji wa hafla hiyo wametoa wito kwa washiriki kujiandikisha mapema kabla zoezi la kujiandikisha kusitishwa ifikapo Februari 7, 2022 au tiketi zitakapokwisha, ambapo walisema uandikishaji wa mio za kilomita 5 utaendelea hadi Februari 26, mwaka huu.

“Kutakuweko na vituo vya kuchukulia namba za ushiriki ambapo Dar es Salaam itakuwa ni eneo la Mlimani City, Arusha hoteli ya Kipo Palace na Moshi katika chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU)”, ilisema taarifa ya waandaaji hao na kuongeza kuwa zoezi hilo litaanza mapema Februari, mwaka huu.

Kwa mujibu wa waandaaji hao, kwa mara ya kwanza kutakuweko na maonesho yanayojulikana kama Kili Expo (The People’s Expo) ambapo wadhamini na wadau wengine wa mbio hizo watapata fursa ya siku tatu za kuonyesha bidhaa na huduma wanazotoa, maonyesho ambayo yanatarajiwa kufanyika kati ya Februari 24-26, 2022, katika viwanja vya MoCU.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 27, 2022, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo zimeandaliwa na taasisi ya Kilimanjaro Company Limited na kuratibiwa na wadau wa hapa nchini kampuni ya Executive Solutions Limited.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles