27.6 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mbio kutumika kudumisha ikolojia Serengeti

Na Mwandishi Wetu

ZAIDI ya watu 500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki mbio za marathon zilizopewa jina la Serengeti Migration Marathon 2020 zinazotarajiwa kufanyika Septemba 6, mwaka huu, wilayani Serengeti. 

Mbio hizo mbali na kutangaza utalii, pia  zinatarajiwa kuleta fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Mji wa Mugumu wilayani Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mbio hizo zinaandaliwa na Serengeti Tourism Sports Agency (SETSA), ambapo mkurugenzi wake  Geoffrey Werema, anasema lengo kuu la tukio hilo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi endelevu na kutangaza utalii kutokana na umuhimu wa ikolojia ya Serengeti kwa maendeleo ya sekta ya utalii na nchi kwa ujumla.

Anasema mbio hizo za Serengeti Marathon zimeasisiwa kutokana na mambo mbalimbali yanayopatikana ndani ya uoto wa Serengeti ikiwamo hifadhi bora duniani yenye maajabu kadhaa likiwamo tukio kubwa la kila mwaka linalohusisha uhamiaji wa nyumbu wanaoambatana na wanyama wengine kama vile pundamilia kutoka kusini mwa hifadhi hiyo kuelekea Masai Mara nchini Kenya.

Anasema licha ya ukweli kwamba eneo hilo limekuwa kivutio kikuu cha watalii kutoka ndani na nje ya nchi, bado linakabiliwa na changamoto ikiwamo migogoro kati ya binadamu na wanyama.

Anasema  zipo shughuli za kibindamu zinazofanywa na wakazi wanaozunguka hifadhi hiyo, ambazo si rafiki kwa ikolojia ya Serengeti na uhifadhi kwa ujumla.

Anasema baadhi ya watu wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya ujangili kwaajili ya kupata kitoweo na kujipatia kipato, jambo ambalo limekuwa likitishia uhai wa uendelevu na uwapo wa moja ya maajabu hayo ya dunia.

Kutokana na hali hiyo, anasema zinahitajika juhudi za pamoja kutoka kwa wadau na Serikali katika kuhakikisha eneo hilo muhimu linatunzwa na kudumu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Werema anasema yeye na wenzake watatu ambao ni wazawa wa Wilaya ya Serengeti, walipoona kuwa wana wajibu wa kutoa mchango wao katika uhifadhi endelevu wa hifadhi hiyo, wamekuja na wazo la Serengeti Migration Marathon ambayo anaamini itaongeza nguvu katika jitihada za mamlaka zilizopo na wadau wengine katika kufanya eneo hilo kuendelea kuwepo.

Anasema baada ya kupata wazo hilo, walisajili tukio hilo Chama cha Riadha nchini na kwamba sasa mbio hizo zitakuwa endelevu na zitakuwa zikifanyika kila Jumapili ya kwanza ya Septemba kila mwaka.

Werema anawaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ambazo kwa sasa zimepata udhamini wa Serengeti lager na Kampuni ya TTCL.

 Anasema mbio hizo zitakazojumuisha ukimbiaji wa  kilimota 5.2, kilimita 10 na 21 na kufanyika mjini Mugumu,  zitahusiaha pia fursa za kutembelea hifadhi ya Serengeti.

 Katika matukio hayo kutakuwa na ujumbe ambao unaolenga kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi endelevu na madhara ya ujangili katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na nini kifanyike ili kuondokana na changamoto hizo na hatimaye ikolojia ya Serengeti iweze kutumika vema katika kutangaza utalii kwa maendeleo ya wakazi wa Serengeti na Taifa kwa ujumla.

Wakizungumzia tukulio hilo baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara, wamesema tukio limekuja muda muafaka na eneo muafaka na kwamba wanaamini kuwa litakuwa na faida kiuchumi na kijamii.

Musa John anasema kuwa kwa muda mrefu shughuli nyingi zinazohusu Serengeti zimekuwa zikifanyika nje ya mkoa wa Mara hivyo kupoteza maana halisi ya shughuli hizo na kwamba wandaaji wanastahili pongezi kwa kuamua kufanya tukio hilo katika eneo husika.

“Kama utakumbuka baada ya Serengeti kutangazwa kuwa hifadhi bora shughuli za kupokea tuzo zilifanyikia Arusha ila tunashukuru kwa juhudi za mkuu  wetu wa Mkoa, Adam Malima  alipambana mpaka sherehe hizo kwa mara ya pili zilifanyika mkoani kwetu ” anasema Musa.


Musa anaongeza kuwa matukio mengi yanayohusu hifadhi ya Serengeti na uendelevu wake yakiwa yanafanyika ndani ya Serengeti anaamini kuwa matukio kama ujangili yatapungua kwa kiasi kikubwa kwavile watu watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa hifadhi hiyo kwa maendeleo yao.

Lydia Manyama mbali ba kuwapongeza wandaaji wa tukio hilo lakini pia anatoa wito kwa wadau wegine kubuni vitu mbalimbali ambavyo vitaamsha ari ya wakazi wa wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara kuona umuhimu wa kushiriki katika kutunza ikolojia ya Serengeti.

Anasema anaamini kuwa mbio hizo zitakuwa endelevu na kwamba zitakuwa na mchango mkubwa katika kukuza utalii mkoani Mara hivyo kuendelea kutoa wito kwa mashirika na makampuni mbalimbali waweze kushirikiana na waandaaji ili ziweze kuwa kubwa zaidi na zenye mafanikio kwani zina mchango mkubwa katika kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya mipaka ya Tanzania

Anasema kuwa mbio hizo zitakuwa ni nembo ya mkoa wa Mara hasa ikizingatiwa kuwa eneo kubwa la hifadhi ya Taifa ya Serengeti inapatikana ndani ya mkoa wa Mara ambapo pia amewaomba watu mbalimbali kujitokeza kushiriki mbio hizo zenye lengo la kuongeza nguvu kafika uhifadhi endelevu lakini pia zitakuwa ni sehemu mojawapo ya kuimarisha afya za washiriki.

Makilagi John anasema matukio kama haya hayana budi kuandaliwa mara kwa mara kwani mbali na kuwa na umhimu katika uhufadhi lakini pia yanasaidia kukuza uchumi wa eneo hilo ambalo kwa miaka mingi limesahaulika ingawa lina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles