Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa klabu ya Mbeya City, umewaonya wapinzani wao, Simba na kuwataka waache kujiamini kwa asilimia kubwa na kupunguza mbwembwe walizoingia nazo mkoani Mbeya, kwani zitaweza kuwagharimu kutokana na maandalizi waliyoyafanya kabla ya kuwavaa katika mchezo wa kesho.
Mbeya City inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 12, watakuwa wenyeji wa Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Akizungumza na MTANZANIA kutoka Mbeya, Ofisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten, alisema wamejiandaa vilivyo kuikabili Simba, huku akiwaonya Wekundu hao wa Msimbazi wasijiamini kupitiliza.
Alisema Simba wanatamba kwa sababu wapo kileleni wakiongoza ligi, lakini wanapaswa kufahamu kuwa kila timu inapambana kuwania nafasi hiyo, ndio maana wamejipanga vyema baada ya nyota wawili wa kikosi cha kwanza waliokuwa majeruhi kurejea kikosini.
“Simba wametua jijini Mbeya wakiwa na mbwembwe nyingi ambazo tumepanga kuzituliza kesho katika mchezo ambao hakika utakuwa mkali na wa kusisimua,” alisema Ten.
Tena alisema kikosi cha Mbeya City chini ya kocha Mmalawi, Kinnah Phiri, kimezidi kuimarika baada ya kurejea kikosini kwa wachezaji, Haruna Shamte na Sankhan Mkandawile ambao walikuwa majeruhi.
Kwa upande wake Ofisa habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, alisema wamejipanga kuendelea kupata matokeo ya ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kuendelea kuongoza ligi.
“Tunashukuru hakuna majeruhi na wachezaji wanayo morali ya hali juu ya kupambana katika mchezo wa kesho ambao utakuwa mgumu kwa kuwa tunacheza ugenini na kila timu inahitaji ushindi,” alisema.