29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mbeba mizigo auawa kwa kisu akigombania Sh 1,500

BEATRICE MOSSES-MANYARA

MKAZI wa Kwere Halmashauri ya Mji wa Babati, Rajabu Said (22), ambaye ni mbeba mizigo, ameuawa kwa kuchomwa kisu chini ya titi la kushoto akigombania kulipwa Sh 1,500 na mwenzake Cleophace John (28) mkazi wa Hangoni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga alisema tukio hilo lilitokea juzi eneo la Kona ya Mrara.

Alisema wabeba mizigo hao walishindwa kuelewana baada ya kubeba begi la abiria aliyeshuka eneo hilo na akawalipa ujira wa Sh 1,500.

Kamanda Senga alidai kuwa Cleophace maarufu kama Mgogo, alikataa kumpa fedha mwenzake ndipo waliendelea kuzozana hali iliyosababisha Rajabu kuchomwa kisu.

Aidha alisema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema walimkimbiza Hospitali ya Mji wa Babati Mrara kwa matibabu ila baada ya muda alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

“Kiini ni ugomvi wa kugombania mgawo wa Sh 1,500 walizopewa na abiria baada ya kumbebea mzigo kutoka stendi ya njia panda ya Mrara hadi stendi ya zamani na mtuhumiwa alikabidhiwa fedha wakiwa wote wawili ili wagawane ila mwenzake aligoma,” alisema Kamanda Senga.

Alidai kuwa mtuhumiwa alipoona anaelemewa, ndipo akachomoa kisu alichokuwa amekiweka kiunoni na kumchoma mwenzake upande wa kushoto na kuanza kukimbia.

“Marehemu alimfukuza mtuhumiwa na kupiga kelele kwamba amechomwa kisu na alimkimbiza umbali wa mita 250 ndipo akaanguka chini baada ya kuishiwa nguvu na ndipo taarifa zikafika polisi,” alidai.

Kamanda Senga alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mji wa Babati Mrara, ukisubiri uchunguzi wa daktari, na mtuhumiwa wa mauaji hayo amekamatwa na yupo kwenye mikono ya polisi kwa taratibu za kiuchunguzi na pindi zikapokamilika atafikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles