22.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Mbaroni kwa kutelekeza watoto shambani

Na YOHANA PAUL-MWANZA

MWANAMKE mmoja anayejulikana kwa jina la Happiness Mafuru (23), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kutelekeza watoto wake wawili kwenye shamba la mpunga.

Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, alisema mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo alfajiri ya Aprili 27, mwaka huu ambapo watoto hao wawili walikutwa kwenye mashamba ya mpunga wakiwa kwenye hali mbaya na hivyo kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Kamanda Muliro aliwataja watoto hao kuwa mmoja ni wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi minne, huku mwingine akiwa wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi saba ambapo kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Muliro alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ikiwamo kumpata mume wa mwanamke huyo ambaye huenda ikawa anahusika kusababisha tukio hilo la kikatili kwa watoto hao ambao walikuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha.

Mbali na hilo, pia alithibitisha kukamatwa kwa watu wawili ambao wanatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya bibi anayefahamika kwa jina la Ndebito Tabita lililotokea Aprili 29, mwaka huu katika Kitongoji cha Imalange, Kijiji cha Mwanangwa wilayani Misungwi mkoani hapa.

Muliro alimtaja mtuhumiwa wa kwanza kuwa ni Rhoda Shaaban (27), ambaye baada ya kuhojiwa kwa kina alikiri kutenda tukio hilo kwa kutumia panga huku mtuhumiwa mwingine ni mganga wa kienyeji Mhangwa Paulo, ambaye anatuhumiwa kwa kupiga ramli chonganishi kuwa bibi huyo ni mchawi na kusababisha kifo chake.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,429FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles