Na Malima Lubasha, Serengeti
NI unyama! Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya mkazi wa kijiji cha Kenokwe kata ya Mosongo wilayani Serengeti mkoani Mara, Rhobi Jumanne kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumnywesha sumu mtoto wa shemeji yake mwenye umri wa miezi miwili na siku 3 (jina linahifadhiwa) huku chanzo cha kufanya hivyo kikiwa bado hakijafahamika bado hakijafahamika.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, ACP Salum Morcase amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo limetokea Julai 19, mwaka huu saa 1 asubuhi katika kijiji cha Kenokwe na kumtaja mwanamke huyo kuwa ni Rhobi Jumanne.
“Tunamshikilia mwanamke huyu kwa tuhuma za kumnywesha motto huyo sumu na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili,” amesema ACP Morcase.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere (DDH), Dk. Edgar Saulo amesema mtoto huyo alipokelewa hapo saa 2.00 asubuhi siku ya tukio akiwa katika hali mbaya na kumpatia tiba ya awali kwa kumuwekea mpira wa kupumua ili kuokoa maisha ya mtoto huyo.
“Kutokana na uchunguzi uliofanyika mtoto huyo ilibainika alinyweshwa sumu ambayo ni dawa kupulizia wadudu wa pamba hali ambayo inaelezwa kusababishwa na ugomvi wa kifamilia, hata hivyo ili kuokoa maisha yake tumempeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kwa matibabu zaidi,” amesema Dk. Saulo.
Ilikuwaje
Kulinganga na Dk. Saulo, mtoto huyo ambaye ni wa kwanza kuzaliwa katika familia hiyo, alinyweshwa sumu wakati ambao wazazi wake walikuwa shambani wakilima.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Elizabeth Nchama(21) amesema yeye na mume wake Baraka Mchuma(21) wanaoishi Kitongoji cha Gosebe Kijiji cha Kenokwe waliondoka alfajiri kwenda shambani na kumuacha mtoto huyo akiwa amelala huku mwangalizi akiwa ni wifi yake aitwaye Yunuis Mchuma.
“Tukiwa tunaendlea na shughuli zetu shambani, ghafla alikuja mlezi wa mtoto(Yunis) akiwa anakimbia wote tulihamani, tukamuuliza kunanini, ndipo akatueleza kuwa “mtoto amenyeshwa dawa ile ya Dipu ya pamba na povu linamtoka mdomoni.
“Tulimuuliza aliyefanya hivyo ni nani, akatueleza kuwa ni mtuhumiwa(Rhobi), kwamba alifika nyumbani na kuingia ndani alikokuwa amelala mtoto na ndipo baada ya muda mfupi hali hiyo ikajitokeza.
“Baada ya taarifa hiiyo tuliacha kulima na kukimbia hadi nyumbani na kumchukua mtoto kumpeleka zahanati ya Mosongo kupata huduma ya matibabu na kushauriwa kumleta hospitali kubwa DDH,” amesema.
Elizabeth alidai kuwa waliwahi kugombana na mtuhumiwa ambaye ni mke wa shemeji yake Jumanne Mchuma akimlalamikia kuwa anamchukulia mume wake jambo ambalo amesema siyo kweli.
Wakizungumza hospitalini hapo mashuhuda na ndugu wa familia hiyo wamesikitishwa na kitendo hicho cha mtoto mdogo kunyweshwa sumu kwamba huo ni ukatili mbaya ambao haukubaliki popote.