22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mbaroni kwa kujifanya askari wa JWTZ

ERICK MUGISHA na SAIDI IBADA (TUDARCo)-Dar es Salaam

MKAZI wa Tabata Segerea, Dar es Salaam, David Ramadhani (33) anayedaiwa kujifanya askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), amepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, kwa makosa mawili, likiwemo la kukutwa na vifaa vya umma.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, ASP Hamisi, akimsomea mashtaka mbele ya Hakimu, Joyce Moshi, alidai Julai 19 eneo la Makao Makuu JKT Mlalakua wilayani Kinondoni, kwa nia ya udanganyifu mshtakiwa  alijitambulisha kuwa ni MP wa Jeshi la Wananchi.

Katika shtaka la pili, anadaiwa Julai 19 katika eneo la Makao Makuu ya JKT Mlalakua, alikutwa na vifaa vya umma kinyume na sheria.

Vifaa hivyo ni sare kamili za askari, sare za askari za kijani, beji na vyombo vya askari, kofia ya askari, kofia ya askari wa usalama wa barabarani, sare za viatu za askari, pingu na redio call.

Mshtakiwa alikana shtaka na ASP Hamisi alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo.

Hakimu Moshi alisema dhamana ipo wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu wenye kusaini bondi ya Sh 2,000,000 kila mmoja, barua za utambulisho na nakala ya vitambulisho.

Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yake itakapotajwa tena Septemba 2.

Katika hatua nyingine, watu wawili wamepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa mashtaka mawili ikiwemo kujaribu kutenda kosa.

Waliofikishwa mahakamani ni raia mmoja wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sengi Kodaso (42), mkazi wa Mbezi Jogoo na Otto Maruma (44), mkazi wa Upanga.

Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Frank Mushi, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Yussuf Aboud, alidai kati ya Agosti 10 na 13, mwaka huu, eneo la Kijitonyama wilayani kinondoni, watuhumiwa walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili, Agosti 13, mwaka huu, eneo la Kijitonyama wilayani Kinondoni, Dar es Salaam watuhumiwa  walijaribu kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa walikana kutenda kosa na mwendesha mashtaka wa Serikali, Aboud alisema hakuna pingamizi kwa upande wa dhamana kwa washtakiwa na upelelezi unaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles