23.6 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Mbarawa ataka Dawasa kujenga miradi wenyewe kupunguza gharama

Anna Potinus – Dar es salaam  

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (Dawasa), kupanga utaratibu wa kujenga wenyewe baadhi ya miradi ili kupunguza gharama za kuajiri wakandarasi.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 2, wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji saini miradi mikubwa ya maji safi kwa jiji la Dar es salaam na Miji ya Pwani iliyogharimu Sh bilioni 114.5.

Akizungumza katika hafla hiyo, amesisitiza kutumia watu wenye uwezo tofauti ambao watafanya kazi usiku na mchana katika kukamilisha miradi hiyo.

“Miradi mingi mamlaka yenyewe ijenge, kuna baadhi ya miradi ya kutandika bomba Dawasa inaweza kujenga bila ya kutafuta mkandarasi, mfano mzuri ni kule Mamlaka ya maji Mbeya kuna mradi wa Mbalizi wa Sh bilioni tatu wanajenga wenyewe.

“Niwaombe mwenyekiti pamoja na uongozi wa Dawasa sasa tujipange miradi yote hasa ile ya vijijini tuchukue watu wetu wakaanze kujenga wenyewe tuna watu wenye uwezo tofauti ninaamini tukifanya hivyo itatusaidia sana,” amesema.

Aidha, Profesa Mbarawa pia amesema kuendelea na utaratibu wa kumpa mkandarasi kila kazi sio jambo jema kwani iwapo wasipopewa malipo yao ya mwanzo hawafanyi kazi na kwamba iwapo watashindwa kuwatumia watu wa kawaida yeye atawachukua na kuwapeleka maeneo mengine.

Miradi iliyowekwa saini ni pamoja na mradi wa usambazaji maji utakaoanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hadi Bagamoyo, mradi wa kusafirisha maji kutoka Jet hadi Buza, kazi ya usimamizi katika visima vya Kimbiji na Mpera, Mradi wa usambazaji maji wa Kisarawe hadi Pugu, mradi wa maji katika Mji wa Mkuranga na mradi wa kusafirisha maji kutoka Mlandizi hadi Chalinze.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,070FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles