Safina Sarwatt, Kilimanjaro
Wananchi katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, leo wamepatwa taharuki baada ya Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kupita barabarani wakiwa wamebeba silaha za moto huku magari yakipeperusha bendera nyekundu, kuzunguka maeneo mbalimbali ya manispaa ya Moshi.
Hali hiyo ilisababisha kusimama kwa shughuli za uzalishaji mali zaidi ya masaa matatu katika maeneo hayo ambapo askari hao waliokuwa wamevalia mavazi maalumu walikuwa wakitembea kwa miguu huku magari yao yakiwa yanapepea bendera nyekundu.
Akizungumzia suala hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah amesema Jeshi la Polisi mkoani humo wamekuwa wakifanya mazoezi ya kawaida na kwamba uwepo wa maaskari hao hakumaanishi kuna tatizo.
“Hali ni shwari ni askari walikuwa wanafanya mazoezi tu ya kawaida ya nadharia, leo walikuwa wanapasha tu kwa sababu hawakufanya mazoezi kwa muda mrefu na kesho wataendelea,” amesema.