27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

MAZOEZI NI SEHEMU YA MATIBABU YA MSONGO WA MAWAZO

 

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.

KATIKA maisha tunayoishi hivi sasa, ni vigumu mno kuepuka msongo wa mawazo au kwa lugha ya Kiingereza stress. Ikumbukwe kwamba, wakati mwingine ni muhimu kwa msongo wa mawazo au stress kutokea kwa muda mfupi, kwa kuwa hutuwezesha kufanya kazi kwa ufasaha na kutupa uwezo wa kumaliza kazi zinazotukabili au hata kushindana inapohitajika kufanya hivyo. Ni stress ndiyo hukuwezesha kumaliza kazi nyingi ulizonazo. Bila hivyo ungefanya kidogo na kusema nitamalizia nyingine kesho, na kujikuta kila siku unafanya kidogo bila kumaliza.

Kisayansi msongo wa mawazo husababishwa na kuongezeka kwa kichocheo kinachoitwa cortisol katika damu kitu ambacho hubadilisha ufanyaji kazi wa mwili ili kukabiliana na mkusanyiko wa kazi au majukumu mengi. Kwa maana hiyo, kichocheo hiki huitwa stress hormone au kichocheo cha msongo wa mawazo. Kama tulivyokwisha kueleza hapo awali, kuongezeka kwa kichocheo hiki kwa muda mfupi ni muhimu na salama kwani hutuwezesha kukabiliana na mawazo na majukumu mengi ndani ya muda mfupi, kitu ambacho hakikwepeki katika maisha.

“Tatizo ni pale kiwango cha cortisol, au kichocheo cha stress kinapokuwa katika kiwango cha juu kwa muda mrefu. Mara nyingi hii hutokana na mtu kushindwa kukabiliana na msongo wa mawazo. Katika hali ya kawaida msongo wa mawazo si tatizo, tatizo ni kushindwa kukabiliana nao.”

Mazoezi yanasaidia vipi?

Katika kila siku ya maisha kiasi cha kichocheo hiki huongezeka kutokana na vitu mbalimbali. Mojawapo ya vitu ambavyo huongeza kiwango cha cortisol au kichocheo cha stress, ni kuwa na kazi au mawazo mengi. Kazi au mawazo mengi huufanya mwili wako kutengeneza kiasi kikubwa cha cortisol ambayo pamoja na vitu vingine husababisha utengenezwaji wa sukari katika mwili. Nia ya sukari hii ni kutengeneza nguvu ya ziada kukabiliana na kazi au mawazo mengi. Endapo kazi au mawazo yatapungua kutokana na kuweza kukabiliana nayo, kiwango cha cortisol pia kitashuka na msongo wa mawazo utaondoka.

Lakini mara nyingine watu hukabiliwa na mawazo na kazi nyingi kwa muda mrefu kiasi cha kushindwa kukabiliana nayo. Katika hali hii, kiwango cha cortisol hubaki juu kwa muda mrefu, kitu ambacho si kizuri kiafya.

“Tafiti za kisayansi na hata zile za kijamii zimethibitisha uwezo wa mazoezi katika kushusha kiwango cha cortisol na hivyo kuzuia madhara ya kiafaya yanayoweza kusababshwa na msongo wa mawazo.

Lakini pia kufanya mazoezi hutoa fursa ya kupumzika kutoka katika kazi au mawazo yasiyoisha, ambayo huweza kusababisha ongezeko la cortisol kwa muda mrefu. Unapokwenda kwenye mazoezi unaondoa ile hali ya kuwaza hivyo kushusha kiwango cha cortisol au kichocheo cha msongo wa mawazo.

Wakati huo huo mazoezi huongeza kiwango cha vichocheo vya furaha mwilini. Kuongezeka kwa vichocheo vya furaha hupunguza mawazo na moja kwa moja kuondoa msongo wa mawazo.

Mazoezi yanayoshauriwa

Mazoezi ya aina zote tatu ni muhimu, ila mazoezi ya aerobics kama kukimbia husaidia kuongeza kiwango cha vichocheo vya furaha kwa kiasi kikubwa. Kwa maana hiyo inashauriwa kufanya mazoezi ya aina hii kwa wingi. Mazoezi ya kulainisha na kunyoosha viungo yakiwamo yale ya yoga ambayo pia husaidia kupumzisha ubongo, husaidia kwa kiasi kikubwa kushusha kiasi cha kichocheo cha msongo wa mawazo (cortisol), pia kuongeza kiwango cha vichocheo vya furaha. Mazoezi ya kusukuma au kunyanyua uzito au resistance exercises husaidia kuongeza kiasi cha kichocheo kinachoitwa testosterone–kichocheo muhimu cha nguvu na uwezo wa kufanya kazi.

Inashauriwa pia kufanya michezo unayoipenda na kufanya mazoezi pamoja na marafiki au ndugu. Tafiti zinaonyesha kwamba kujumuika kwa aina yoyote husaidia kuzuia na kupunguza msongo wa mawazo.

Kumbuka kwamba msongo wa mawazo hutokana na sababu za kibaiolojia, na mazoezi yanayo sehemu kubwa katika kuzuia na kukabili tatizo hili. Hakikisha unafanya mazoezi mara kwa mara ili kukabiliana na msongo wa mawazo kiurahisi zaidi.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa kutumia 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles