Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.
HAKUNA ubishi kwamba mazoezi ni sehemu muhimu sana kwa mtu mwenye ugonjwa wa kisukari, lakini ifahamike kwamba, kwa mtu mwenye aina ya kwanza ya kisukari au kisukari kinachotegemea insulin (type 1 diabetes mellitus) kufanya mazoezi kunahitaji uangalifu zaidi. Kwa maana hiyo basi, maelezo yafuatayo yatawahusu zaidi wale wenye kisukari kisichotegemea insulin. Dondoo kwa ajili ya kisukari kinachotegemea insulin zitaelezewa katika sehemu nyingine.
Jipangie mazoezi unayo yapenda
Kumbuka mazoezi si kwenda gym peke yake, au kucheza mpira na michezo mingine. Mazoezi ni pamoja na kazi za nyumbani, kutembea, kuendesha baiskeli na hata kucheza dansi na ngoma. Kitu chochote kinachoifanya misuli yako kufanya kazi, na nguvu ya mwili kutumika ni mazoezi tosha. Chagua mazoezi unayoyapenda iwe ni kucheza dansi au kutembea. Cha muhimu hakikisha unafanya mazoezi kwa muda usiopungua nusu saa kwa siku. Ukiweza kufanya mazoezi hayo mfululizo kwa dakika 30 mara moja ni sawa, lakini kumbuka kwamba unaweza kuugawanya muda huo na kufanya mazoezi kwa dakika kumi kumi, ili mradi ndani ya saa 24 utimize nusu saa au dakika 30.
Pata muongozo wa daktari
Ni kawaida kabisa kupata muongozo wa kiasi na muda wa kutumia dawa (prescription) tunapokuwa wagonjwa, lakini tunachosahau ni umuhimu wa kupata muongozo kama huu kwa ajili ya mazoezi na lishe. Muulize daktari wako kuhusu mazoezi ikiwa ni pamoja na kiwango, muda na mambo muhimu ya kuzingatia. Ikiwezekana akuandikie kabisa (exercise prescription) au akupeleke kwa daktari wa maoezi.
Vaa kipima mwendo (motion sensor)
Kipima mwendo ni kifaa kinachoweza kupima kiasi cha hatua ulizotembea katika siku. Viko vipima mwendo vya aina nyingi (pedometer and accellerometers) na hata vile vyenye uwezo wa kukadiria kiasi cha nguvu iliyotumiwa na mwili wako (accelerometer). Tafiti zinaonyesha kwamba kuwa na kipima mwendo husaidia kutoa hamasa hivyo kukutia moyo wa kufanya mazoezi. Jiwekee malengo ya kutembea hatua zaidi ya 10,000 kwa siku, hata kama usipozifikisha kwa kufahamu hatua ulizotembea utapata moyo wa kufanya mazoezi zaidi.
 Fanya mazoezi ya kuipa nguvu misuli na mifupa angalau mara mbili kwa wiki
Mazoezi ya kutumia nguvu kama kunyanyua au kusukuma vitu vizito (resistance exercise) ni muhimu sana kwa mtu mwenye ugonjwa wa kisukari kisichotegemea insulin. Vyama vingi vya ugonjwa wa kisukari duniani vinashauri kufanya mazoezi ya aina hii angalau mara mbili kwa wiki. Mazoezi haya husaidia kudhibiti sukari kwenye damu. Unaweza kunyanyua vitu vizito, kuvuta kamba za mpira au kutumia mashine maalumu. Unaweza pia kufanya push ups au mazoezi ya kuchuchumaa na kusimama (squats) kwa kutumia uzito wa mwili wako mwenyewe.