MAZIWA NI TIBA MBADALA YA SONONA

1
1549

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


RIPOTI iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha zaidi ya watu milioni 300 wanaugua ugonjwa wa sonona (depression).

Shirika hilo linaeleza kwamba kati ya mwaka 2005 hadi 2015 kuna ongezeko la zaidi ya asilimia 18 ya watu wanaougua ugonjwa huo.

Wataalamu wa afya ya akili wanasema ni ugonjwa ambao huathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda (msongo wa mawazo).

Wanasema ugonjwa huo humsababishia muhusika kuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, kidesturi, na nyanja nyingine za kijamii.

Tabia hizo huathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) pamoja na kuathiri uhusiano wake katika jamii hatimaye huathiri jamii nzima inayomzunguka.

 

Maziwa ni tiba

Mtaalamu wa Lishe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Elizabeth Liymo anasema maziwa hasa yatokanayo na wanyama yana uwezo wa kukabili hali hiyo.

“Maziwa ni kinywaji muhimu na cha kipekee kinachosaidia kujenga afya ya mwili wa binadamu. Ni kinywaji ambacho kinahusishwa na afya bora, kina  virutubisho mbalimbali ambavyo ni muhimu kwa miili yetu,” anasema.

Mtaalamu huyo anasema maziwa mazuri zaidi ni yale yanayotokana na wanyama kwani yana protein yenye ubora wa hali ya juu.

Anasema maziwa yatokanayo na wanyama pia yana ‘utajiri’ mkubwa wa kirutubisho cha vitamin D ambayo husaidia utengenezwaji wa kichocheo serotonin.

 

Faida yake

Anafafanua kwamba, serotonin ni kichocheo ambacho kinahusiana na mambo ya ‘mood’, hamu ya kula na kulala.

“Kichocheo hiki husaidia mwili kukabili hali ya msongo wa mawazo, (stress/depression), ikiwa mtu anakabiliwa na hali hiyo mara kwa mara anashauriwa kunywa maziwa  hasa yatokanayo na wanyama,” anasema.

Anasema kwa kawaida mwili ukipunguza kirutubisho cha vitamin D wakati mwingine huhisi mwili wake kuwa mchovu na kukosa raha.

“Hivyo akinywa kinywaji hiki mara kwa mara humsaidia kukabili hali hiyo ya uchovu na kukosa raha,” anasema.

Pia anasema yana madini ya calcium kwa wingi ambayo ni muhimu kwa afya ya mifupa kwani husaidia kuzuia ugonjwa unaoitwa kitaalamu oesteoporosis.

Anasema vitamin D iliyopo ndani ya maziwa husaidia pia kuimarisha afya ya meno ya mwanadamu.

Anasema husaidia kuimarisha afya ya moyo na hivyo kumwepusha mtu kupata tatizo la shinikizo la juu la damu.

“Maziwa yana madini ya potassium ambayo yenyewe husaidia kutanua mishipa inayokwenda kwenye moyo, kitendo hicho husaidia damu kupita kwa urahisi jinsi inavyotakiwa,” anasema.

Mtaalamu huyo anasema protein inayopatikana katika maziwa husaidia mno katika utengenezaji na uimara wa misuli ya mwili.

“Kazi ya protein ni kujenga mwili… hupatikana pia kwenye nyama, maini au vyanzo vyote vya wanyama, ni tofauti na inayopatikana kwenye maharagwe na vyakula vingine.

“Kiwango cha protein huwa kinatofautiana baina ya chanzo kimoja na kingine, lakini inayopatikana kwenye maziwa inapatikana kwa ubora wa hali ya juu, huwa tayari ina amino acid zote muhimu zinazohitajika mwilini.

Anasema maziwa pia ni chanzo cha nishati iliyopo katika mfumo wa mafuta ambayo huzuia misuli kuweza kutumia nishati yake.

“Yenyewe ‘naturally’ yana mafuta ambayo moja kwa moja husaidia misuli yetu kutotumia zile nguvu zake kwa wingi,” anafafanua.

Anasema ingawa maziwa yatokanayo na wanyama ni bora zaidi katika kujenga afya ya mwanadamu, hata hivyo wapo baadhi ya watu ambao hawawezi kabisa kunywa maziwa hayo.

“Kitaalamu hawa wanakabiliwa na tatizo liitwalo lactose intolerance. Yaani wamezaliwa miili yao ikiwa haina kichocheo kiitwacho lactose,” anasema na kuongeza:

“Lactose ni kichocheo ambacho husaidia katika umeng’enywaji wa maziwa, kichocheo hiki husaidia kuvunja vunja sukari iliyopo katika maziwa.

“Mtu ambaye hana kichocheo hiki akinywa maziwa na ikatokea akatapika, maziwa hayo hutoka yakiwa hayajaganda, mtu mwenye hiki kichocheo akitapika maziwa huwa tayari yameanza kuganda,” anasema.

Anasema mtu ambaye hana kichocheo hiki mara nyingi akinywa maziwa wakati mwingine huharisha.

 

Ushauri

Anasema kwa kuwa watu hawa wanakabiliwa na mzio(allergy) wa maziwa, huwa wanashauriwa kunywa maziwa yatokanayo na vyanzo vingine.

 

Hali ya unywaji maziwa nchini

Tanzania inatajwa kuwa na jiografia nzuri ya malisho ya wanyama na inashika nafasi ya pili katika nchi zenye mifugo mingi baada ya Ethiopia.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Chakula Duniani inaeleza hivyo, hata hivyo inaonesha bado kiwango cha unywaji maziwa nchini kipo chini.

Shirika hilo linapendekeza wastani wa unywaji maziwa kwa mwaka ni lita 200 kwa kila Mtanzania, lakini inakadiriwa hunywa lita 47 pekee sawa na milimita 131.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tale Olenasha anasema hali hiyo huchangia watoto wengi kupata tatizo la udumavu, ambapo takwimu zinaonesha asilimia 34 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana tatizo la udumavu kutokana na kutokunywa maziwa na kukosa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha.

Anasema hali hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu Afrika kwa kiwango kikubwa cha watoto wenye udumavu, ikitanguliwa na Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Uchumi wa Taifa hauwezi kuimarika wakati watoto wake wakiwa hawana afya bora inayoweza kuwafanya wakafikiri vizuri na kuwa wabunifu katika shughuli wanazozifanya, kila mwaka serikali inatumia Sh milioni 650 kugharimia matatizo yanayotoka na ukosefu wa lishe bora,” anasema.

Anasema ni wakati mwafaka Watanzania kuamka na kuanza kunywa kinywaji hicho ambacho kina faida katika kujenga afya ya mwanadamu.

1 COMMENT

  1. Ninawashauri watanzania kuwa natabia yakufuga has a wale kwenye uwezo wakufuga ng’ombe wa biashara wawekeze uko kwa wing I ili kupata maziwa halisi nasio hayo wanayo chakachua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here