MAZITO BUNGENI: NAPE AKOSOA MRADI WA STIGLER’S GORGE, ADAI HAUPO KWENYE ILANI CCM, MBUNGE Z’BAR ARUSHA KOMBORA

1
798

Na FREDY AZZAH-DODOMA


HOJA nzito zimezua mjadala ndani ya Bunge, huku wabunge wa CCM wakinyukana baada ya Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, kuhoji hatua ya Serikali katika utekelezaji wa mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge, ambao haupo katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Pamoja na hayo, Serikali imetangaza neema kwa watumishi wa Serikali 1,370, wenye vyeti vya darasa la saba kurudishwa kazini.

 

NAPE ASHANGAA Stigler’s Gorge

Akichangia hotuba ya mapato na matumzi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Nape, ameishangaa Serikali kuweka nguvu nyingi kwenye mradi wa Stigler’s Gorge aliosema haupo kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chao ya mwaka 2015.

Alisema kwa sasa inaonekana Serikali inataka kuachana na mradi wa gesi ambao waliunadi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Nape, alihoji Serikali kama kuacha mpango wa uchumi wa gesi si kuisaliti ilani ya CCM na wananchi wa Lindi na Mtwara.

Mradi wa Stiglers Gorge unatarajiwa kuzalisha megawati 2,100, huku unaozalishwa na gesi kutoka Mtwara, Kinyerezi I inazalisha Megawati 185 na II inazalisha megawati 240.

“Tulipopiga kura 2015, tuliamini sana uchumi wa gesi ni mkombozi mkubwa na uko salama mikononi mwa Rais Magufuli (Rais John Magufuli) na Serikali ya awamu ya tano.

“Ndio ulikuwa mkataba wetu na siyo kwa maneno, uliwekwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukurasa wa 75 mpaka 77, eneo kubwa sana limezungumzwa uchumi wa gesi,” alisema Nape.

Alisema kura nyingi alizozipata Rais Magufuli ni kwa sababu ya makubaliano hayo yaliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na atakwenda kuyatekeleza.

“Kwa summary (ufupi), moja ilikuwa kuendelea kujenga miundombinu ya kuendeleza huu uchumi wa gesi kwa Lindi na Mtwara.

“La pili ilikuwa kuwaandaa wananchi wanufaike na kufaidika na gesi na mafuta kwa Lindi na Mtwara na lipo jambo mahusisi la ujenzi wa LNG plant (mtambo wa kuchakata gesi) kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ili limo kwenye Ilani ya Uchaguzi.

“Lakini nasikitika sana nilipoangalia hotuba ya Waziri Mkuu, kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho hakuna neno gesi kabisa, na inaonekana hata ukienda eneo lenyewe shughuli mbalimbali zinazoendana na gesi kwa Lindi na Mtwara, ni kama vile zimeanza kufungwa na shughuli imesimama kabisa.

“Kwa sababu naona jitihada kubwa zinaanza kwenda kwenye Stiglers, umeme wa maji, mimi sina matatizo nayo, yawezekana huo ndio uamuzi, lakini Stiglers kwenye Ilani haimo.

“Ilani tumezungumza gesi, nishati ya gesi, tena kwa sehemu kubwa sana na hii ndiyo ilikuwa imani ya wana Lindi na Mtwara kwa Serikali ya awamu ya tano,” alisema.

Nape alisema zilikuwapo jitihada zilizofanywa na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi hadi mradi wa Songosongo ukapatikana na kwamba Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, nao walifanya jitihada ikiwamo kuinua uchumi wa gesi.

 “Kwa hotuba ya Waziri Mkuu na kwa bahati mbaya tumemkabidhi sisi Magufuli tukaamini tupo salama, alipotupa Majaliwa (Waziri Mkuu Kassim Majaliwa) tukaamini tupo salama zaidi kwa sababu Waziri Mkuu anatoka kwetu.

“Sasa ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani hakuna kabisa kabisa, maana yake ni kwamba hili jambo pengine limeanza kuachwa, sasa tuende kwenye Stiglers, lakini aje hatusaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM? 

“Lakini je, hatuwasaliti wana Lindi na Mtwara ambao walitupa kura na kutuamini kwamba gesi yao na uchumi wao uko salama?” alihoji Nape.

Alisema suala hilo ni bomu kubwa, kwani wakati wa mchakato wa gesi kuanza, hali ya kisiasa na kijamii Lindi na Mtwara ilikuwa tabu.

“Sasa imetulia tukiamini neema ipo, lakini kiuchumi baada ya harakati za gesi na mafuta Kusini, watu walianza kuja kuwekeza, uchumi wa Lindi na Mtwara ukaanza kukua, watu wakaanza kuwekeza.

“Hali ilivyo sasa hivi, watu wameanza kuondoka, uchumi wa Lindi na Mtwara unadorora, hali yetu ngumu sana.

“Sasa mimi nimwombe Waziri Mkuu kwa unyenyekevu sana asikubali suala la gesi lifie mikononi mwake yeye akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania, siyo sawa,” alisema Nape.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

1 COMMENT

  1. Napenda kumpongeza sana Kiongozi kijana jasiri kama huyu Mkuu wa Mkoa wa Dsm kwa kupata mafunuo kila kuchapo. wanaokusema vibaya waache waseme tu lakini songa mbele na MUNGU akusaidie na kukulinda azidi kukupa neema na kibali cha kuongoza hata kwa ngazi za juu zaidi.

Leave a Reply to mary modest shayo Cancel reply

Please enter your comment!
Please enter your name here