30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAZINGIRA YA WAZAZI HUJENGA TABIA YA WATOTO

Na Christian Bwaya,

UMEWAHI kujiuliza wapi tunakojifunza tabia zetu? Kwa nini tunatofautiana? Kwanini, kwa mfano, mtu anaweza akawakuta watu kadhaa wamekusanyika mahali asiwasalimie kwa kuwapa mkono lakini mwingine akampa mkono kila anayemwona? Kwanini wapo watu wasioweza kuongea kwa sauti ya upole lakini wengine wanaweza? Kwanini kuna watu ukimgusa kidogo mnakosana lakini isiwe hivyo ukiwafanyia watu wengine hicho hicho?

Hii ni mifano ya tofauti tulizonazo binadamu. Kuna tabia fulani tunazo lakini tunaweza kushangaa tumezitoa wapi. Mwanamume uliyeoa unakuta unaongea na mke wako kama baba yako alivyokuwa anaongea na mama yako. Unaweza usipende unachokifanya lakini ndivyo ulivyo. Inaweza kukuchukua muda mrefu kubadilika.

 Sheria ya uhusiano katika familia

Kuna mambo mengi yanachangia kutengeneza tabia zetu. Unaweza kurithi tabia fulani kutoka kwa wazazi wako hata kama wao hawaonekani kuwa nazo. Mfano ni hasira. Wapo watu wana hasira kali hata kama wazazi wao ni wapole. Upo ushahidi wa kiutafiti kwamba hasira inaweza kuwa kwenye vinasaba vya urithi. Pamoja na hayo, ipo nafasi kubwa ya mazingira ya malezi. Mahali ulikokulia, aina ya wazazi waliokulea wamekufanya uwe vile ulivyo.

Watoto wanapozaliwa wanakuta familia yenye mfumo wa sheria zisizoandikwa. Tangu ulipozaliwa, ulikutana na sheria fulani zinazoongoza namna utakavyofanya mambo yako. Kwa mfano, unaweza kuamini ni lazima kuonesha uso wa tabasamu unapoongea na mwenzako. Kutabasamu inakuwa ni sheria ya familia. Kinyume chake pia kinawezekana.

Matendo karibu yote tunayoyafanya yanaongozwa na sheria tuliyoikuta kwenye familia. Wapo watu wakiamka, shughuli ya kwanza kufanya ni kusali. Hawawezi kuondoka kitandani bila kusali. Ndio sheria ya maisha yake. Lakini wapo pia wanaoamka bila kusali. Wanafuata sheria isiyoandikwa.

Hiyo ni baadhi ya mifano inayoweza kuonesha namna gani maisha yetu ya kawaida yanavyoongozwa na sheria isiyowazi. Namna ya kusalimia watu, namna ya kuongea na watu, namna ya kusema unachofikiri, namna ya kupokea kile unachopewa. Yote haya yanaongozwa na sheria zisizoandikwa. 

Nafasi ya uhusiano wa wazazi

Unaweza kujiuliza, nani huandika sheria hizi kwenye familia? Jibu ni wazazi ndio watunzi wa sheria hizi. Kile kinachofanywa na mzazi hugeuka kuwa sheria kwenye moyo na ufahamu wa mtoto. Nikupe mifano.

Namna gani baba na mama wanaongea, wanawasiliana, wanazungumza wao kwa wao, hutengeneza sheria zitakazoongoza uhusiano wa watoto wao. Mzazi anayeomba msamaha pale anapomkosea mwenzake, anawafundisha watoto sheria muhimu ya familia kwamba unapokosea unaomba msamaha. Kuomba msamaha kunaingia kwenye vichwa vya watoto kwa sababu ndicho wanachokiona kikifanywa na wazazi.

Baba anapokuwa na tabia ya kuongea kwa kufoka, anawafundisha watoto kuwa huwezi kuongea bila kufoka. Baba huyu anaweza kuwafundisha watoto kufanya kinyume chake kwa maneno. Lakini kitakachosikilizwa na mtoto ni kile anachokifanya mzazi. Matendo ya mzazi yanakuwa ndiyo sheria itakayomwongoza mtoto.

Unawafundisha nini watoto wako?

Kile unachokifanya mzazi kina nguvu kubwa ya kuwa sheria kwa wanao. Unachokifanya ni somo kamili kwa mtoto. Unaweza ukafikiri mtoto ni mdogo mno kuelewa. Fahamu kwamba mtoto anajifunza kwako kimya kimya. Unaongea nini, unafanya nini, unavaa nini, unapenda nini yote hayo ni somo muhimu kwa mwanao. Una kila sababu ya kuwa makini na nini unachoongea na kumfanyia mwenzako. Ukifanyacho ni sheria.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles