26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

MAZINGIRA SAHIHI YA KUFANYIA MAZOEZI

 

 

Dk. Fredirick L Mashili, MD,PhD.

UMEWAHI kujiuliza ni kwanini ufanyapo mazoezi kwenye mazingira ya baridi na ukavu, unakuwa na nguvu zaidi ukilinganisha na pale unapofanya mazoezi kwenye mazingira ya joto na unyevu nyevu? Ukifahamu hili hutashangaa sana ni kwanini watu hulipa fedha nyingi kwenda kwenye gyms zenye kiyoyozi saa zote na kupuuzia zile za bei rahisi, zisizo hata na feni.

Hii imenitokea mara nyingi mno. Niko gym nafanya mazoezi anaingia mtu na kuniomba tuzime air conditioner (AC). Namuomba kama anadhani ni muhimu kufanya hivyo basi tufungue madirisha ili hewa iingie. Anaonekana kutoridhika, kasha anatoa sababu isiyo niingia akilini–eti chumba kinatakiwa kiwe na joto ili atokwe jasho jingi, kwa imani kwamba atakuwa amepunguza uzito mwingi kiurahisi zaidi.

Kwa maana hiyo basi, leo tutajadili mazingira muafaka ya kufanyia mazoezi na kutoa shahidi za kisayansi kusisitiza umuhimu wa mazingira hayo.

Kiukweli, kufanyia mazoezi nje (outdoor) ndiyo njia salama na yenye faida nyingi kwa afya na malengo mengine. Hii inatokana na ukweli kwamba, nje kuna hewa ya asili ambayo hutupa oksijeni ya kutosha kutengeneza nguvu tunayohitaji kwaajili ya mazoezi na hata kuchoma mafuta.   Hewa hii ambayo huzunguka bila bugdha, husaidia pia kuondoa hewa chafu ya carbon dioxide (CO2) kwa haraka zaidi.

Lakini ni muhimu kukubaliana na ukweli kwamba, kutokana na sababu mbalimbali hatuwezi siku zote kupata fursa ya kufanyia mazoezi nje na hivyo kulazimika kufanyia mazoezi ndani. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia tunapoamua kufanyia mazoezi ndani.

Hakikisha kuna hewa ya kutosha

Mazoezi yanahitaji nguvu, na nguvu hutokana na virutubisho ambavyo kwa lugha rahisi, huchomwa kwa kutumia hewa ya oksijeni na kutoa nguvu tunayoihitaji. Lakini pia kama nia ni kupunguza uzito kwa kuchoma mafuta, hewa ya oksijeni ndiyo hufanya kazi hiyo. Fahamu kwamba unapofanya mazoezi kwenye chumba kisicho na hewa ya kutosha utachoka haraka hivyo kushindwa kutimiza muda unao tosha kuvuna faida za mazoezi hayo.

Hakikisha hakuna hali ya unyevuunyevu (high humidity)

Tunapofanya mazoezi tunatokwa na jasho. Kazi ya jasho ni kuupooza mwili ili uendelee kufanya kazi. Kupoozwa huku hutokea pale jasho linapobadilika na kuwa hewa hivyo kukauka (evaporation). Endapo mazingira unayofanyia mazoezi kuna hali ya unyevunyevu (high humidity), huwa ni vigumu kwa jasho kubadilika kuwa hewa kitu ambacho husababisha jasho lisifanye kazi yake ya kupooza mwili. Hii itakusababisha utokwe na jasho jingi na nguo zako kuloana chapachapa, kitu ambacho watu wengi hujidanganya kuwa ni kizuri. Kuwapo kwa hali ya unyevunyevu, huuchosha mwili. Kuruhusu hewa kuingia ndani husaidia sana katika hili, maana hewa huwa kavu na husaidia kukausha jasho na kuupooza mwili. Hii hukupa nguvu na uwezo wa kuendelea kufanya mazoezi.

Hakikisha kuna mwanga wa kutosha

Mwanga si kwa ajili tu ya kuona, bali husaidia kuhamasisha ubongo na kukupa nguvu ya kuendelea. Kuona kila kitu kilicho katika chumba cha mazoezi ni msingi muhimu pia katika kuzuia kuumia na kupata majeraha wakati wa mazoezi.

Tumia vitendea kazi mwafaka

Vaa nguo na viatu vizuri vya mazoezi vinavyoendana na mazingira. Ni jambo la kushangaza ila la kawaida kabisa kumkuta mtu amevaa koti (jacket) wakati wa mazoezi hata katika hali ya joto. Hii yote hutokana na imani kwamba kutokwa jasho jingi kuna maanisha kuvuna faida zaidi za mazoezi, wakati kiukweli jasho lisilokauka hukufanya uchoke mapema. Mazoea haya yanatokana na ukweli kwamba watu wengi huiga vile wanavyoviona kwenye runinga na magazeti, ambayo huonyesha watu wakifanya mazoezi katika mazingira ya baridi sana. Ikumbukwe kwamba hata katika nchi za baridi, kuna nguo za mazoezi kwa msimu wa baridi na zile za msimu wa joto.

Nini cha kufanya

Ukiweza fanyia mazoezi nje.

Lakini kama hili haliwezekani, ni muhimu kupangilia vizuri chumba cha kufanyia mazoezi na kitu cha msingi kuliko vyote ni uwapo wa hewa ya kutosha na hali ya ukavu. Kama hewa haingii ndani ni muhimu kuwa na viyoyozi vya kutosha na hivi hutakiwa kufanya kazi wakati wote. Viyoyozi husaidia kuzungusha hewa ndani ya chumba kwa kuingiza hewa safi na kutoa ile iliyo chafu.

Dk. Mashili ni mtaalamu wa fisiolojia ya mazoezi na homoni. Pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa kutumia: namba 0752255949, barua pepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea moja wapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles