Mayay amtaka Zahera abadili mbinu za vita

0
613

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

BAADA ya timu ya Yanga kupangwa na Pyramids FC ya Misri, hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo, Ally Mayay amesema mbinu za kocha, Mwinyi Zahera ndizo zitakazoamua hatima ya timu hiyo.


Yanga itamenyana na Pyramids Octoba 27, mwaka huu, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa  kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho  utakaochezwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Timu hizo zitarudiana Novemba 3, mwaka huu mchezo utakarindima Uwanja wa June 30, Cairo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mayay alisema Yanga inaweza kuwasukuma nje ya Waarabu hao, iwapo tu Zahera atakuwa na mbinu mbadala za kuwabana wapinzani wake.

Alisema kama Mkongomani huyo anataka kufanikiwa , anatakiwa kwanza kupata ufumbuzi wa tatizo la ubutu wa safu yake ya ushambuliaji,  ili iwe na uwezo wa kuvuna mabao ya kutosha.

“Tunajua Yanga ina mchezo mgumu dhidi ya Pyramids, lakini kwenye mpira hakuna kinachoshindikana, inategemea tu umejipanga vipi, ubora na thamani ya kikosi cha wapinzani si kigezo cha kupata ushindi.

“Kitu pekee kinachoweza kuisadia Yanga ni mbinu za Zahera, anatakiwa kubadilika kwa kiasi kikubwa, tunajua ana tatizo la ushambuliaji ambalo toka waondoke Ibrahim Ajib na Herietier Makambo amekosa mbadala,”alisema.

Alisema  baada ya kuwakosa wachezaji wakucheza kama walivyokuwa Ajib na Makambo, Zahera anapaswa kuingia na mfumo mwingine ambao utamwezesha kuvuna mabao ya kutosha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here