27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Mayanja kutumbua majipu Simba

abdi-banda-390x390*Apanga kuanza na Banda, amchokoza ataka afukuzwe

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, amepanga kutumbua majipu ndani ya klabu hiyo, huku akieleza kuanza na kiungo wa timu hiyo, Abdi Banda, ambaye amemchosha kutokana na tabia za utovu wa nidhamu anazozifanya mara kwa mara.

Mganda huyo ameweka wazi kuwa hatakuwa tayari kuendelea kumfundisha mchezaji huyo kwenye kikosi chake, baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu kwenye mchezo wao dhidi ya Coastal Union ya Tanga, kwa kugoma kufuata maelekezo aliyompa, ambapo alimwambia ajiandae kuingia kuchukua nafasi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, aliyekuwa uwanjani, lakini mchezaji huyo aligoma kuingia.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mayanja alisema licha ya suala hilo kuwapo kwenye kamati ya nidhamu ya klabu hiyo, anaomba mchezaji huyo afukuzwe  kwenye klabu hiyo, vinginevyo ataondoka yeye.

“Sijawahi kumfundisha mchezaji mwenye utovu wa  nidhamu kama huyu tangu niwe kocha, hivyo hana hadhi ya kuwapo kwenye kikosi changu.

“Hakuna mchezaji ambaye ana tabia chafu kama huyu, aliwahi kufanya vitendo hivi akiwa chini ya kocha Seleman Matola, Dylan Kerry na sasa mimi, ambapo anakwenda kwenye mitandao ya kijamii anatuma ujinga akitaka watu wamtetee, lakini akae akijua kwangu amegonga mwamba,” alisema Mayanja.

Mayanja aliongezea kuwa hatua hiyo ya kutumbua majipu itakuwa endelevu, kwa kuwa anataka kuhakikisha anaisafisha timu  hiyo ili kila mchezaji awe na nidhamu.

“Banda ni jipu, nahofia asijewaambukiza wengine tabia zake, lazima aadhibiwe awe wa mfano ili tabia hii isiendelee kwa wachezaji wengine na kama ikitokea kwa mwingine atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa,” alisema Mayanja.

Hata hivyo, Mayanja alionesha kufurahishwa na tabia ya mchezaji wa timu ya Azam FC, John Bocco na Haruna Niyonzima wa Yanga, akieleza wameonesha ukomavu  wa soka kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Bocco amekuwa majeruhi kwa muda mrefu, ingekuwaje  kama angekuwa kiburi, Niyonzima muangalie alikosa, alipogundua makosa yake akaomba msamaha na akasamehewa, hukukuta anagombana au kuendeleza tabia za utovu wa nidhamu.

“Mchezaji hata kama atakuwa na uwezo mkubwa uwanjani, bila nidhamu ni kazi bure, hawezi kupata mafanikio yoyote bila kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, ndiyo maana nataka kuisafisha timu hii, ili wachezaji waweze kuwa makini na jambo hilo,” alisema Mayanja.

Kwa upande wake Banda, alisema kuwa hatishwi na kauli za kushambuliwa na kocha wake, yeye anasubiri Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo iweze kumuadhibu.

“Uongozi kupitia kamati ya nidhabu ndio wenye mamlaka dhidi yangu, hadi sasa bado hawajanimbia chochote, ila namshangaa Kocha anavyozungumza kwenye vyombo vya habari wakati uongozi bado haujatoa maamuzi,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles