Na Johns Njozi, Dar es Salaam
Kampuni ya Maxcom Africa (Max Malipo), imekanusha taarifa kuwa mkataba wake na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) unamalizika hatua itakayosababisha kampuni hiyo kushindwa kutoa huduma ya kuuza umeme wa LUKU kupitia kwa mawakala wa Maxmalipo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa kampuni hiyo, Deogratous Lazari taarifa hizo zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza hayo, si za kweli.
Amesema taarifa hizo zinasema baada ya Machi 31, mwaka huu Wananchi na wabia wa Maxcom wataendelea kujipatia huduma mbalimbali kupitia kwenye mfumo wa Maxmalipo ikiwamo huduma ya LUKU hazina ukweli wowote na hali halisi.
“Kilichotokea ni kwamba, tumeunganishwa kwenye mfumo wa serikali wa malipo kielektroniki (GEPG), hivyo baada ya Machi 31, wananchi na wabia wetu wataendelea kujipatia huduma mbalimbali ikiwamo ya LUKU kupitia Maxmalipo.
“Hivyo, tunapenda kuwahakikishia wananchi kwamba, malipo ya huduma ya LUKU na huduma nyingine zitaendelea kupatikana kupitia kwa mawakala na wabia wote wa Maxmalipo nchi nzima,” amesema Lazari katika taarifa yake hiyo.
Aidha, kampuni hiyo imeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wabia na wananchi wanaotumia huduma ya Maxmalipo.