26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Maximo kuifikisha Yanga anga za TP Mazembe

Marcio Maximo
Kocha mpya wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Marcio Maximo

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

KOCHA mpya wa timu ya Yanga, Mbrazil Marcio Maximo, ameeleza kuwa amekuja Yanga kwa kazi ya kuijenga timu hiyo kufikia ubora wa kimataifa na kutisha Afrika, kama ilivyo timu ya TP Mazembe.

Mbrazil huyo aliwahi kuinoa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ miaka minne iliyopita na kuiwezesha kufahamika kimataifa kutokana na kiwango bora kilichokuwa kikioneshwa na timu hiyo kipindi cha uongozi wake na kuzisumbua timu vigogo Afrika.

Maximo, aliyetua juzi mchana nchini akitokea nchini kwao Brazil, amesaini mkataba wa miaka miwili na msaidizi wake, Leonardo Neiva, ambapo amepewa majukumu mawili ya kuwa kocha mkuu wa timu hiyo na jukumu la kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.

Akizungumza jana kwenye makao makuu ya timu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam, Maximo, aliyeambatana na msaidizi wake, Neiva, alisema TP Mazembe inajulikana kwa ajili ya uwekezaji walioufanya kwa kusajili wachezaji bora wa kimataifa, hivyo atajenga misingi bora Yanga ya kuinyanyua timu hiyo.

“Najisikia furaha kuteuliwa kuwa kocha wa Yanga, naiheshimu sana Tanzania kwani watu wa hapa walinipa kitu zaidi ya maisha. Nimekuja Yanga kuijenga si tu ndani ya uwanja kwa kushinda, bali hata nje ya uwanja, nataka kuifanya iwe na ubora kama wa TP Mazembe ambayo inasifika kimataifa, kikubwa naomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki.

“Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa sasa ni bora na ya upinzani tofauti na miaka ya nyuma niliyokuwepo hapa, kipindi kile ubingwa ulikuwa unawaniwa na timu mbili tu, Yanga na Simba, ila hivi sasa zipo Azam FC na Mbeya City ni timu ngeni, naziheshimu timu hizo ila nimekuja kufanya kazi ya kuifanya Yanga kuwa bora zaidi,” alisema Maximo.

Katika hatua nyingine, Maximo alisema ugomvi wake na Kaseja uliotokea alipokuwa akiifundisha Stars umekwisha, kwani kilikuwa kipindi kilichopita na sasa anafungua ukurasa mwingine.

“Chuji alikuwa hapa na ameondoka kwenye timu na Kaseja yupo, sitaki kuyaleta mambo yaliyopita, bali kwa sasa tunafungua ukurasa mpya, yote hayo yamepita Kaseja ni kipa mzuri na ana uzoefu na sasa nataka kumtumia kumpa changamoto Dida kwenye kikosi change,” alisema.

Maximo alisema ataanza rasmi programu yake Jumatatu kwa kuwanoa wachezaji wachache wa Yanga walioanza mazoezi, ambao atawapa mazoezi  ya kuwajenga stamina kwa mazoezi ya nguvu na kuwajenga kiufundi na ataanza kuwapa mbinu pindi wachezaji waliopo timu za Taifa watakaporejea.

Akizungumza kwa ufupi, msaidizi wake, Neiva ambaye pia amepewa mikoba ya kuwa kocha msaidizi wa timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Yanga, alisema amemjua Maximo muda mrefu alipokuwa kocha wake kipindi cha nyuma na sasa amejumuika naye kama kocha na kuahidi kumpa ushirikiano katika kuijenga Yanga.

Naye Wakala wa Maximo, Ally Mleh ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Manyara Sports Management,  alisema alikuwa na mawasiliano ya miaka mitatu iliyopita na kocha huyo na haikuwa rahisi kwa Maximo kutua Yanga, kwani alikuwa akitakiwa na timu nyingine kutoka China, Ethiopia, Malawi na Afrika Kusini.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu naye alisema kuja kwa Maximo na Neiva ni lengo lao la kuijenga upya Yanga kufikia hatua ya kimataifa, huku akidai kuna mengine makubwa zaidi yanakuja kutimiza mipango hiyo.

Wakati huo huo, kiungo mpya mshambuliaji wa Yanga, Mbrazil Andrey Coutinho ametua nchini jana saa 8.30 mchana na kulakiwa na baadhi ya mashabiki wa Yanga na kueleza kuwa amekuja kushindana tu, huku akieleza kuifahamu timu hiyo kupitia mitandao na leo asubuhi ataongea na waandishi wa habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles