
Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam
AMEBANWA! Sahau kuhusu ule uhuru wa kuongea na vyombo vya habari aliokuwa akipewa Kocha Mkuu wa Yanga SC, Marcio Maximo wakati akiinoa Taifa Stars miaka minne iliyopita, hivi sasa hali ni tofauti baada ya kubanwa na kunyimwa uhuru huo.
Maximo ameshasaini mkataba wa miaka miwili kuinoa Yanga, sambamba na msaidizi wake Leonardo Neiva na jana wameanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi hicho, asubuhi kwenye ufukwe wa bahari wa Coco na jioni katika Uwanja wa Bandari, uliopo Tandika.
Mbrazil huyo alikataa kuongea na waandishi wa habari jana kwenye mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika Coco, akidai anabanwa na vipengele vya mkataba baina yake na Yanga vinavyokataza kuzungumza ovyo na vyombo vya habari.
“Naheshimu kazi yenu kiukweli, ila siwezi kuongea chochote kwani nabanwa na mkataba, nitakuwa nikiongea na waandishi pale klabu itakapoandaa mikutano kwa mujibu wa mkataba, vilevile baada ya mechi…‘Tupo pamoja tutafika’,” alisema kwa ufupi Maximo.
Hali hiyo ya kubanwa kwa Maximo ni tofauti kabisa na alivyokuwa Stars, kwani alikuwa akipata uhuru mkubwa wa kuongea na waandishi na kufanikiwa kujenga umoja kwa Watanzania kuipenda Stars, kupitia uwezo wake mkubwa wa kuhamasisha na kuifanya timu hiyo kupiga hatua kubwa kisoka.
Maximo ameleta utaratibu mpya Yanga, kwa wachezaji na benchi la ufundi kusali pamoja kabla ya kuanza mazoezi na wakati wa kumaliza, ambapo jana asubuhi MTANZANIA Jumatano lilishuhudia utaratibu huo kwenye mazoezi yaliyoanza majira ya saa 2.30 na kumalizika saa 3.30 asubuhi katika ufukwe wa Coco.
Katika mazoezi hayo yaliyosimamiwa kwa kiasi kikubwa na Neiva, yalihusisha wachezaji wa timu kubwa na ya vijana, waliwafanyisha mazoezi ya nguvu kwa muda wa saa moja kwa lengo la kusaka pumzi na kujenga mwili.
Moja ya mazoezi hayo ni kuruka koni na wachezaji kubebana kimgongo mgongo pamoja na kukimbia raundi moja kwa umbali mrefu kwenye ufukwe huo.
Mbali na mazoezi hayo, Maximo alipata wasaa kuongea na wachezaji Jerryson Tegete, Juma Kaseja ambaye wamemaliza bifu lao na baadhi ya viongozi wa benchi la Ufundi.
Wachezaji wa timu kubwa waliofanya mazoezi ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na Juma Kaseja, Juma Abdul, Swaleh Abdallah, Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Salum Telela, Omega Seme, Hassan Dilunga, Said Bahanuzi, Andrey Coutinho, Hussein Javu, Nizar Khalfan na Jeryson Tegete.
Kibarua cha kwanza cha Maximo ni kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame, linalotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi ujao jijini Kigali, Rwanda, vilevile ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.