24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Mawaziri wawili wajibizana mtandaoni

Mwandishi wetu-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Muungano, January Makamba na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, wameibua mnyukano katika akaunti zao za mtandao wa Twetter.

Kiini cha mnyukano wa mawaziri hao, ni taarifa ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) juu ya kuanzisha aina mpya ya utalii Mlima Kilimanjaro.

Mvutano huo ulitokana na mmoja wa watumiaji wa Twitter kuweka kwenye ukurasa wake link ya taarifa ya Tanapa ikisema; “Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), inatarajia kuanzisha usafiri mpya wa kutumia magari ya umeme yanayopita kwenye nyaya (Cable Cars) kupeleka watalii Mlima Kilimanjaro.”

Baada ya andiko hilo, January alijibu link hiyo kupitia Twitter akisema; “inabidi watu wa mazingira tupitishe na kutoa cheti kwanza kabla hawajaanza. Na tutafanya ‘studies’ ili kujua ‘impact’ kwa mazingira na uthabiti wa ‘mitigation measures’.”

Kutokana na ujumbe huo, Kigwangalla naye aliibuka na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa watu wa mazingira wanataka kuingilia kati mradi huo wa Cables Cars Kilimanjaro.

“Watu wa mazingira wanataka kuingilia kati mradi wa Cables Cars Kilimanjaro. Lengo letu ni kukuza utalii, kuongeza mapato na kuboresha ‘experience’ ya watalii wetu nchini.

“Tusipokuwa wabunifu tunatukanwa kutokutumia vizuri vivutio vyetu, tukiamka wanakuja na ‘speed governors’ (vidhibiti mwendo),” aliandika.

Katika tweet yake nyingine, Kigwangalla aliandika; “mlolongo wa ‘regulative mechanisms’ zimeua biashara zetu na kukwamisha uwekezaji kwa muda mrefu sana hapa nchini. Hivi sasa tunajaribu kuondoa vikwazo ili kukuza uwekezaji na uchumi wetu. Nchi zinazokua kwa kasi zimeepuka sana njia hizo za kimagharibi.”

Aliandika pia kwamba;“hivi kuna nchi ngapi zimeweka Cables Cars kwenye milima yake? Hizi haziharibu mazingira? Cable inapita juu inaharibu mazingira gani? Zaidi ya ekari 350,000 za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni risk kubwa? Watu wa mazingira wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano tu.”

Kutokana na maandiko ya mawaziri hao, mtumiaji mwingine wa mtandao huo anayejiita  Mabuga J Chananja aliandika; “nafikiri ingekuwa busara zaidi kukutana na watu wa mazingira myajenge kwa pamoja badala ya ku-tweet, haisaidii.”

Kingwangalla alimjibu akiandika; “wao wame-tweet, hawakuleta barua, majibu ya suala la kwenye mtandao yanatolewa mtandaoni kwani unadhani sisi tungefanya mradi huu bila kuangalia sheria za mazingira?

“Mlima tumehifadhi wenyewe miaka yote saa 24, leo tufanye kitu cha kuuharibu? Ama ni dharau na kujionesha tu.”

Baada ya andiko hilo la Kigwangalla, mchangiaji mwenye jina la Muuza Asali, alimwandikia January akisema; “bro (kaka) punguzeni makongamano.”

Makongamano ni hoja aliyoiibua Kigwangalla, ikatafsiriwa kuwa ni kijembe kwa January, kwamba wao wamekalia makongamano.

January naye alimjibu mchangiaji huyo akisema; “baada ya kuona ujumbe huo katika blog, nikaweka wazi kile ambacho sheria inahitaji. Itakuwa ni kukosa ukomavu kwa upande wangu kujibu hadharani, kubishana au kumshambulia mwenzangu ambaye anajitahidi kufanya mambo yawe mazuri kwenye eneo lake”.

Katika mjadala huo, baadhi ya wachangiaji walionekana kumpongeza January kwa kuonesha ukomavu, huku wengine wakimweleza Kigwangalla kuwa mradi huo unaondoa maana halisi ya kupanda mlima.

Mchangiaji wa mtandao huo anayejitambulisha kwa jina la Kilimang’ombi, aliandika; “ubunifu sawa, lakini haupaswi kudhoofisha controls (udhibiti) tulizoweka wenyewe. JMakamba, hata hivyo nakupongeza sana. Wewe ni mmoja kati ya mawaziri bora kabisa msimu huu.”

Kigwangalla alimjibu akiandika; “Controls zina faida gani kama hakuna ugali kwenye meza ya Mtanzania?”

Mchangiaji mwingine anayeitwa Majesh Bakari, aliandika; “itapendeza ukae na anko JMakamba na wadau wengine wa mazingira na utalii mje na kitu kimoja cha kujenga na chenye matokeo chanya baina ya pande mbili.”

Kigwangalla alimjibu kwa kuandika; “vikao vinachelewesha maendeleo! Mtu akiweka kikwazo tunaachana na mradi, tunafanya mengine. Kazi zipo nyingi na muda ni mchache. Tunataka kufikia mwakani tufikishe watalii 2,000,000. Mradi mmoja ukituchukulia muda hatutoweza.”

Mwingine anayejiita Ayub N, aliandika; “hatukatai cable cars ndani ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro, lakini vipi ajira za vijana zitakazoathiriwa na huu mradi, umejipangaje kuzipatia mbadala wake?”

Kigwangalla alimjibu; “ajira zitaongezeka wala siyo kupungua. Watalii wa cable cars ni tofauti na wa hiking.”

Mchangiaji mwingine anayeitwa Charles Sululu, alimuunga mkono Kigwangalla akisema; “sidhani kama ina madhara kimazingira kwa sababu umeme hautoi hewa ya ukaa! hapo ni ujenzi wa nguzo tu na cable.

“Hii itainua utalii maradufu, kuna wasiomudu kupanda kwa nguvu zao, lakini wakisaidiwa na lift watatimiza ndoto zao na pesa itaingia, ila pia msifunge njia za miguu.”

Kigwangalla alimjibu wa kifupi; “sawa kabisa.”

Gazeti hili liliwatafuta mawaziri hao kupitia simu zao za kinganjani, lakini hawakupokea na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hawakujibu.

Juni 7 mwaka huu, Kigwangalla aliwaondoa hofu waongoza watalii na wapagazi juu ya mradi wa kutumia gari maalumu za umeme (Cable Cars) kupandisha watalii Mlima Kilimanjaro.

Alisema mradi huo utakuwa na lengo la kusaidia makundi maalumu kama walemavu kukaribia kuona kilele cha mlima huo na kamwe haitarajiwi kuondoa ajira kwa vijana au kuharibu ikolojia ya mlima huo.

“Hii ni ‘products’ (bidhaa) mpya katika kuongeza watalii kupanda Mlima Kilimanjaro, lakini haitavuruga utaratibu wa watalii kupanda mlima kwa kutembea,” alisema.

Awali, mwenyekiti wa tuzo wa waongoza bora watalii, Christopher Nzela, aliomba kuitishwa kikao maalumu cha ufafanuzi wa jambo hili kwa sababu linawapa hofu.

Alisema kuna taharuki kuwa mradi huo unakwenda kuondoa ajira kwa Watanzania wengi pamoja na biashara ya utalii, ndiyo sababu wanataka kushirikishwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wapagazi Tanzania (TPO), Loshiye Mollel, alisema mradi huo unawapa hofu ya kupoteza zaidi ya ajira 10,000 za wapagazi.

“Kuna zaidi ya wapagazi 20,000 wanaotegemea kazi ya kuwapandisha mlima watalii, ambayo huchukua wastani wa siku saba, hivyo mradi ukianza mtalii atapanda siku moja gari,” alisema.

Alisema wanataka ushirikishwaji wa mradi huo ambao kama ukitekelezwa bila umakini pia utashusha mapato ya utalii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles