27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri watangaza operesheni ya wafugaji Kigoma

Editha Karlo, Kigoma

WIZARA tano zilizokuwa na kikao maalumu mkoani Kigoma kwa siku mbili mfululizo, zimefikia makubaliano rasmi kuendesha operesheni maalumu ya pamoja ya kuwandoa wafugaji na wakulima wanaodaiwa kuishi na kufanya kazi katika maeneo ya misitu na hifadhi mkoani Kigoma.

Hatua hiyo, inakuja baada ya operesheni kama hiyo kusitishwa mwishoni mwa mwaka jana, baada ya vurugu zilizozuka eneo la Mpeta wilayani Uvinza ambapo wananchi kadhaa walidaiwa kuuawa wakiwamo polisi wawili.

Waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

Wengine ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (mazingira), Mussa Sima na makatibu wakuu wa wizara hizo.

Waziri Jafo alisema Serikali imetoa muda kwa wakulima walioomba kibali maalumu ili wavumiliwe hadi wavune mazao yao na kwamba ndani ya miezi sita operesheni hiyo inapaswa kuwa imefanyika.

“Serekali itaendesha operesheni kubwa kuondoa uvamizi wa wakulima, wafugaji na watu wengine wanaofanya shughuli zisizo za halali kwenye misitu na mapori yaliyohifadhiwa kisheria  zikiwemo hifadhi za misitu za halmashauri za wilaya na vijiji”alisema.

Alisema Serikali imemega jumla ya hekta 10 kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini kwa ajili ya kilimo na mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambapo hekta 2,174 zimetolewa kwa Kijiji cha Mvinza, hekta 2,496 zimetolewa kwa Kijiji cha Kagerankanda.

Waziri Jafo, alisema wizara ya mifugo na uvuvi imetenga  hekta 20,000 kutoka maeneo mbalimbali ya  mkoa huo  kwa ajili ya ufugaji wenye tija  pia Serikali itaendea kutafuta maeneo mengine kwaajili ya wafugaji.

“Wahamiaji haramu kutoka nje ya nchi nao wamekuwa wakichangia katika uharibifu wa misitu na mapori, wahamiaji hao haramu wataondolewa nchini mara moja,” alisema.

Katika tamko lao hilo pia wamezitaka mamlaka za serikali za mitaa ambazo zina mashamba ambayo hayajaendelezwa zihakikishe taratibu za ubatilisho wa miliki hizo umefanyika ili  ardhi itakayopatikana ipangwe kwa matumizi ya kilimo na ufugaji wenye tija.

Waliutaka pia uongozi wa mkoa na wilaya uhakikishe kuwa usafirishaji wa mifugo unazingatia sheria ya utambuzi,usajili na ufuatiliaji wa mifugo namba 12 ya mwaka 2010.

Pia wametaka wananchi wote waliovamia eneo lililokuwa kwenye mpango wa uanzishwaji wa vitalu vya ufugaji na mashamba katika Halmashauri ya Uvinza watapangwa na mamlaka husika kwa ufugaji na kilimo chenye tija baada tathimini iliyoelekezwa na waziri wa mifugo kukamilika.

ATHARI

Waziri Jafo alisema tathmini iliyofanyika katika mkoa huo, imeonyesha hifadhi za misitu na mapori ya akiba yamevamiwa kwa shughuli za kilimo, ufugaji, ukataji miti kwa ajili ya nishati na ujenzi na makazi ambapo baadhi ya vijiji vimesajiliwa ndani ya maeneo hayo.

Alisema uvamizi huo umesababisha athari kama sehemu kubwa ya hifadhi za misitu na mapori ya wanyamapori kupoteza uoto wake wa asili, kuharibika kwa vyanzo vingi vya maji, ikiwamo mito mikubwa (mfano Mto Malagarasi) na kupungua kwa bioanuai.

Nyingine ni kuongezeka kwa matumizi ya dawa za mifugo katika hifadhi ambayo yanasababisha kuchafuka kwa vyanzo vya maji na kuua viumbe hai na ongezeko la mmomonyoko wa ardhí na kusababisha mito na mabwawa kujaa udongo.

Nyingine, ni tishio la kuzuka kwa magonjwa hatari kutokana na mwingiliano wa mifugo na wanyamapori katika maeneo yaliyohifadhiwa, ikiwamo kimeta (anthrax), midomo na miguu (FMD), kichaa cha mbwa (rabies), malale (sleeping sickness).

Taarifa zinaonesha viumbe hai mbalimbali vilivyokuwa vinapatikana katika hifadhi hiyo kabla ya uvamizi huo kuongezeka vimepungua au kutoweka kabisa.

Kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimesababisha kupungua ubora wa malisho ya wanyamapori pamoja na kuathiri upatikanaji wa mvua za uhakika na hivyo kutishia uhakika wa chakula na kuongezeka kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles