30.4 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Mawaziri waparurana bungeni

 RAMADHAN HASSAN – DODOMA 

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe juzi amewasha moto bungeni akihoji kwa waziri mwenzake wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi vilipo viwanja vyake alivyonunua. 

Mnyukano huo ulianza mara baada ya wabunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu wa mwaka 2020. 

Lukuvi kudai kwamba Jiji la Dodoma limepima viwanja 10,000 hivyo mbunge yeyote ambaye anataka kiwanja aende Jiji au amuone yeye. 

“Jiji la Dodoma wamejitahidi sana, wamepima viwanja zaidi ya 10,000 tumeuza mpaka hapa kila mtu anajua, Naibu Waziri wangu alikuwa na fomu hapa alikuwa anazunguka nazo za kuuza viwanja. 

“Hapa ndani wakati nasoma bajeti ya mwaka juzi waliomba niwaongezee miezi mitatu kwa ajili ya kulipa, watu wamenunua viwanja vitatu, vinne mpaka vitano. 

“Leo (juzi) nataka kukwambia wale wenye mawazo yako (Spika) wana Guest House, wana Apartment hapa, nawajua, mtu anafanya biashara 

“Na nataka kuwahakikishia hata anayetaka kiwanja aende Jiji akikosa aje kwangu, vipo viwanja vya kumwaga, hapa ndio mahala pake, kwa Mtanzania wa kawaida hata mbunge hapa ni ‘second home’ (nyumba ya pili),” alisema Lukuvi. 

Kutokana na kauli hiyo, ilimzilamu Waziri Kamwelwe, kusimama na alidai kwamba siku ambayo Lukuvi alitangaza uuzwaji wa viwanja miaka mitatu iliyopita, yeye alilipia siku ileile viwanja viwili, lakini hadi sasa bado hajavipata. 

Kamwelwe alihoji kama yeye ikiwa ni waziri hajapata viwanja vyake je, Mtanzania wa kawaida itakuwaje. 

“Mheshimiwa Spika, mimi nilipewa ofa nikalipia viwanja viwili siku hiyo hiyo, shahidi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mavunde (Anthony), mpaka leo (juzi) sijapata kiwanja, tena mimi ni waziri nimeongea kwa mkuu wa mkoa nimeongea kwa mkurugenzi na naibu waziri huyu (Mavunde) sijapata kiwanja mpaka leo (juzi), nimelipa hela zote,” alisema Kamwelwe. 

Akijibu hoja hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema; “Very interesting, hicho kiwanja Mheshimiwa Waziri nitafuatilia mimi, nitahakikisha unapata kiwanja, asante sana kwa kunipa taarifa muhimu.” 

WABUNGE KUHAMISHWA 

Awali Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, aliomba mwongozo kwa Spika wa Bunge kuhusu wabunge kuondolewa katika nyumba na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA). 

“Mheshimiwa Spika, baadhi ya wabunge wako hapa leo wamepokea barua kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa TBA kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwamba waondoke haraka katika nyumba za Serikali ambazo wanakaa katika maeneo mbalimbali. 

“Sasa Mheshimiwa Spika tuombe mwongozo wako, wabunge kazi wanazofanya ni ngumu sana na wakati mwingine zinahatarisha usalama wetu na wengine ni viongozi. 

“Asilimia 99 ni wabunge wa chama tawala, nikuombe Spika kwa kazi kubwa wanayoifanya na Bunge lipo Dodoma, hivyo wanastahili kuwa katika sehemu salama, nikuombe waziri atusaidie wasubiri mpaka uchaguzi utakapokamilika ndiyo tupatiwe barua. 

“Tumwombe Mheshimiwa Waziri atambue na yeye ni mbunge, mamlaka aliyopewa ni ya kumsaidia tu Mheshimiwa Rais kama sisi na niombe mwongozo mwezi Novemba tutakuwa wabunge wa kawaida mpaka Rais atakapoteua Baraza la Mawaziri,” alisema Mchengerwa. 

Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri Kamwelwe alisema wapo wabunge ambao wanalipiwa kodi na Bunge na wengine wanajilipia wenyewe, hivyo jambo hilo halikutakiwa kuletwa bungeni. 

“Nilivyoingia hapa bungeni wapo wachache walikuja kunipa taarifa, Wakala wa Majengo ya Serikali Tanzania, ina kazi mbili; moja ni kutoa huduma kwa wananchi na nyingine wanafanya biashara. 

“Katika mazungumzo na wabunge, wapo wabunge ambao wameingia mikataba kwa makubaliano kwamba Bunge ndiyo litakuwa likiwalipia kodi ila wapo wengine watalipa wao moja kwa moja. 

 “Kwa sababu hili suala ni la kimkataba, wabunge wale wanaolipiwa na Bunge, Bunge litaisha mwezi wa sita kwa vyovyote vile kulikuwa kuna hoja kwamba mikataba yao itaisha ndiyo maana wakajihami. 

“Ila wale ambao hawalipiwi na Bunge siwajibu moja kwa moja ile mikataba na wakati mikataba inaingiwa haikuletwa hapa bungeni kwa hiyo niwaombe tu wabunge na mimi mwenyewe nimo nimesaini mkataba na mkataba wangu ulikuwa ni wa kulipa moja kwa moja na nikipata barua nitawajibu kwamba mimi nipo, hili ni suala dogo sana,” alisema Kamwelwe. 

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema; “Yaani mnachoambiwa wabunge Dodoma ndiyo kwenu, Dodoma ndio makao makuu ya nchi, kwa hiyo jengeni, hakutaka kusema tu mheshimiwa Waziri. 

“Kwa anayekwama kiwanja basi muoneni Mheshimiwa Jafo (Selemani), manaibu mawaziri wapo, na Tamisemi ndiyo wanaosimammia Jiji la Dodoma. 

“Lakini mnaokosa viwanja yupo Mheshimiwa Lukuvi, yeye ndiye anayepima viwanja na sijui safari hii kwanini imekuwa hivi. Mwaka 2000 tulikuwa tunagaiwa na Mheshimiwa Lukuvi, wengi walikataa, nakumbuka hata mimi cha kwangu,” alisema Ndugai. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,873FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles