NA ESTHER MNYIKA – DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema kuanzia sasa mawaziri wote wanatakiwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti kwa kila mwezi kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO), Hassan Abas, alisema hiyo ni miongoni mwa mikakati ya Serikali katika kuboresha mawasiliano baina yake na wananchi kwa kuwapatia taarifa za utekelezaji wa ahadi zake.
“Lengo kubwa ni kujua vipaumbele vya bajeti zao ni vipi na namna ya kutekelezwa, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji,” alisema Abbas na kuongeza:
“Kila mwezi waziri atawasilisha taarifa yake popote pale atakapokuwa kupitia vyombo mbalimbali hususani vipindi maalumu vilivyopo kwenye runinga, redio na kufanya mkutano.”
“Mkakati huo utaanza Agosti 25 mwaka huu, ratiba ipo tayari na taarifa hizo za mawaziri zitapelekwa kwenye mifumo ya ndani ya Serikali.”
Alitaja mkakati mwingine kuwa ni wa Idara ya Habari (Maelezo) kueleza kwa umma kila mara na haraka iwezekanavyo utekelezaji wa sekta zote katika ngazi ya taifa.
Aidha, alisema katika kutekeleza hayo wiki ijayo ataanza kufanya ziara ya kushtukiza katika vyombo vya habari vyote nchini kusikiliza changamoto zinazowakabili waandishi wa habari.
Alisema atafanya mazungumzo na taasisi mbalimbali katika kutafuta fursa na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa ajili ya waandishi wa habari.