31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI KUHUDHURIA MKUTANO AU

 

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAWAZIRI na makatibu wakuu wa wizara mbalimbali nchini wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa 28 wa wakuu wa Umoja wa Afrika (AU), unaoendelea jijini Addis Ababa Ethiopia. 

Mkutano huo unaofanyika jijini humo kwa ngazi tofauti, tayari umeanza ukihusisha vikao vya wataalamu.

Katika mkutano wa mwaka jana uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, pamoja na mambo mengine, nchi wanachama ziliafikiana kutuma vikosi vya kusimamia amani vya Afrika katika nchi zinazokabiliwa na machafuko.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, Mindi Kasiga, alisema wajumbe kutoka Tanzania wataondoka kwa awamu kwenda katika mkutano huo.

Kuhusu Rais Dk. John Magufuli kuhudhuria mkutano huo, alisema: “Tayari Rais Dk. Magufuli ana taarifa ingawa bado hajathibitisha kama atakwenda au atatuma mwakilishi katika mkutano huo.”

Katika hatua nyingine, msemaji huyo alisema mazungumzo ya usuluhishi wa mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi yanatarajiwa kufanyika nchini Malawi kuanzia Februari 3 hadi 5.

Mazungumzo hayo yanafanyika kupitia Tume ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi. Kikao cha mwisho kama hicho kilifanyika nchini mwaka 2003.

“Kumekuwa na sintofahamu baina yetu na nchi ya Malawi kutokana na mpaka, sisi kama wanadiplomasia tunaamini kwamba mgogoro huu unaweza kumalizika kwa suluhu ya diplomasia na si vinginevyo.

“Vikao havijafanyika kwa muda mrefu na pengine ndiyo mwanya huu wa kutokuelewana ukaweza kupenya,” alisema Kasiga.

Ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Mahiga na unatarajiwa kuondoka Februari 2 kuelekea Malawi.

Alitaja baadhi ya mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na ushirikiano kiuchumi, hasa katika suala la bandari kwa sababu baadhi ya mizigo ya Malawi inapitia nchini, usafiri wa anga, elimu na mengine.

Malawi imekuwa ikidai Ziwa Nyasa liko upande wake na imelipa jina la Ziwa Malawi na kulijumuisha kwenye ramani yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles